Pages

Thursday, 10 July 2014

MADEREVA 180 WA BODABODA RUMANDE



KUNA vijana waendesha bodaboda 180 waliokamatwa jijini Dar es Salaam na sasa wapo mahabusu, imedaiwa. Wengine 400 wametozwa faini na wengine wamehukumiwa kwa kosa la kuingiza bodaboda katikati ya Jiji.


Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati ya Madereva wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Daudi Laurian.
Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Laurian aliiomba Serikali kuwaachia huru madereva wote wa bodaboda, waliokamatwa kwa kosa la kuingiza bodaboda katikati ya Jiji.
“ Mpaka sasa kuna vijana 180 waliokamatwa na wapo mahabusu na wengine 400 wametozwa faini mpaka sasa na wengine wanahukumiwa kwa kosa hili,” alidai.
Alisema agizo hilo la kutoingia mjini, limesababisha mambo mengi, ikiwemo madereva kuishi kwa hofu ndani ya nchi na madereva kutozwa faini ya fedha nyingi, ambazo ni Sh 50,000, Sh 100,000, Sh 250,000 na Sh 450,000.
Alisema fedha hizo ni nyingi na zinazidi uwezo wa vipato vya madereva hao na zinakinzana na Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchikavu na Majini (Sumatra).
“Fedha hizi zinatozwa, lakini wakati mwingine madereva bodaboda hawapatiwi risiti; na wakati mwingine wanapatiwa risiti feki” alidai Laurian.
Pia, alisema wanaomba agizo hilo la Serikali la kupiga marufuku bodaboda kuingia katikati ya Jiji, lisitishwe, kwani sababu iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki, kuwa bodaboda zinasababisha ujambazi, si za kweli.
Alidai kuwa bodaboda ambazo hazipo kisheria, ndizo zinahusika na matukio hayo ya ujambazi ; na sio bodaboda za kibiashara.
Alisema ili kudhibiti uhalifu na utoaji wa huduma bora, wilaya zote tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni, zina alama za utambulisho wa kimaeneo kwa mujibu wa Kanuni za Sumatra, ambapo Wilaya ya Temeke ni rangi ya Kijani, Ilala rangi Nyekundu na Kinondoni rangi ya Bluu.
Aliomba Serikali kutoa ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo ili kulinda ajira za vijana wengi, ambao kipato chao kinategemea bodaboda.
Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana kwa simu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, kutokana na madereva wengi waliokamatwa na kuwekwa mahabusu, wapo katika eneo lake la Ilala. Mtu mmoja aliyeshika simu ya Kamanda huyo, alijibu kwa kifupi kuwa “ Nimesikia shida yako, nitamwambia yeye”.
Gazeti hili halikuishia hapo, bali liliwasiliana kwa simu na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutokana na polisi wa kanda hiyo, ndio waliokamata na wanaendelea kukamata vijana hao waendesha bodaboda.
Kova alisema kwanza hana taarifa kama waendesha bodaboda, walifanya mkutano wao na waandishi wa habari jana. Pili, Kova alisema hawezi kutoa taarifa ya idadi ya waendesha bodaboda, waliokwishakamatwa na waliopo mahabusu, kwa sababu anayejua hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye ndiye aliyetoa agizo hilo la bodaboda.
Alisisitiza kuwa Mkuu wa Mkoa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na ndiye Msemaji wa suala hilo. Kova alisema Jeshi la Polisi, Halmashauri ya Jiji na halmashauri za manispaa ni watekelezaji tu wa agizo hilo la Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
“Aliyetoa agizo juu ya bodaboda ni Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Mimi siwezi kutoa taarifa juu ya suala hilo. Jeshi la Polisi na Halmashauri ya Jiji tunatekeleza tu agizo hilo. Mtafute Mkuu wa Mkoa umuulize,” alisema Kova saa 11.45 jana jioni.
Aidha, gazeti hili lilijaribu kuwasiliana mara mbili kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki. Alipopokea simu kwa mara ya kwanza, gazeti lilimweleza kuhusu malalamiko hayo ya madereva wa bodaboda na kumuomba atoe ufafanuzi.
Mkuu wa Mkoa aliomba apigiwe baadaye kwa maelezo kuwa yupo hospitali. Alipopigiwa mara ya pili, alisema apigiwe baadaye kwani bado yupo hospitali.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment