Pages

Sunday, 27 July 2014

KUUFANYA MWILI WAKO UWE NA UMBILE ZURI


Watu wengi hupendelea kuwa na maumbo fulani, hasa yale ambayo wengi wanadhani yanavutia mbele za watu.
Uanamitindo ni miongoni mwa fursa zilizofanikiwa kuteka soko la ajira hususani kwa vijana katika upande wa mavazi. Urembo na utashati ndiyo nyenzo inayotafsiriwa kuvutia zaidi ndani ya soko hilo.
Hata hivyo, katika ajira hiyo kuna vigezo mbalimbali ambavyo vinahitajika ili kunufaika na fursa zilizopo. Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na utengenezaji wa maumbile ya mwili.
Walimu mbalimbali wa mazoezi ya kujenga mwili katika maumbile hayo wanasema vijana wengi wamekuwa wakitamani kuwa wanamitindo, lakini wameshindwa kutambua mbinu za kutengeneza miili yao.
Mwalimu wa mazoezi ya viungo, Chiko Yosia anataja hatua zinazohitajika katika kumjenga mwanamitindo wa kiume.
“Kuna kanuni za kufuata katika mazoezi ya mwanamitindo ili asiwe kama baunsa au ‘Body builder’ (mtu anayejenga mwili). Hii ni pamoja na kuhakikisha anafanya mazoezi ya kubeba vyuma vyepesi, kufanya mazoezi ya kukimbia na kuruka kamba,” anasema Chiko.
“Mazoezi ya vyuma vyepesi yatamsaidia kujenga mikono, kifua, mabega, mgongo na miguu.”
Anasema upande wa mazoezi ya kukimbia, yatamsaidia kujenga pumzi, kuondoa maradhi madogo madogo na kupunguza uzito.
“Katika mazoezi ya aerobic steps (viungo), yatamsaidia sana kukata tumbo la chini, juu, pembeni na kati,” anasema.
Chiko anabainisha kuwa kijana mwembamba wa kawaida au wa unene wowote wanayo nafasi ya kubadilika.”
“Kwa mnene, itakuwa kazi kubwa kumbadilisha awe mwanamitindo kwani ni lazima apitie hatua ya kwanza katika kupunguza uzito wake kabla ya kuanza kukata mwili wake ili kuwa mwanamitindo tofauti na mwembamba wa kawaida ambaye inaweza kuwa rahisi,” anasema Chiku.
Pamoja na mkakati huo wa kutengeneza mwili kuwa mwepesi na unaosifika kwa mitindo, anasema mazoezi ni jambo ambalo mtu hapaswi kuliacha.
Akiacha ghafla anaweza kupata madhara ya kupotea kwa umbile lake na kuathirika kiafya ikiwamo kushambuliwa na maradhi. Maradhi hayo ni kama vile kisukari na maradhi ya moyo.”
Mbali na hatua hiyo, Chiku anatoa tahadhari ya kuzingatia katika ratiba ya kupata lishe bora, muda wa mazoezi na utumiaji wa maji ya moto kwa kunywa.

No comments:

Post a Comment