Bado kuna ubishi mwingi kwa mashabiki wa soka kuhusu ubora wa mabeki wa pembeni wanaocheza Ligi Kuu Bara.
Wengi wanaamini beki wa kulia wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ ndiye aliwahi kuitendea haki nafasi ya beki wa pembeni. Mchezaji mwingine anayetajwa kuitendea haki nafasi ya ulinzi ni beki wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe.
Kapombe ambaye sasa ataichezea Azam kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao aliwahi kufanya majaribio kwenye klabu ya AS Cannes Ufaransa.
Akizungumzia majaribio hayo, Kapombe anasema,“Nilichukuliwa hapa kwenda Uholanzi kufanya majaribio, lakini nilipofika nikapata nafasi Ufaransa kwenye timu ya AS Cannes nikafanya majaribio siku tatu na ile timu ikakubalina na mimi kwamba wanisajili.
“Lakini kilichokuja kutokea baadaye ni kwamba walivunja makubaliano yetu kwani wao walikubaliana na Simba wanitoe mimi bure halafu nikiuzwa kwenye timu nyingine ndipo Simba watapata asilimia fulani na kweli nikasaini miaka miwili, lakini ile timu haikufanya kama vile tulivyokubalina kwenye mkataba hasa katika mshahara,”anasema Kapombe.
Anasema,”Ujue lilipotokea lile tatizo ilinichukua muda mrefu kuamua na wakati huo huo nilikuwa namsikiliza kwanza wakala wangu, pia Simba walikuwa wanakuja kunishauri, lakini wengi walinishauri nirudi katika ile timu mimi nikawaambia nitawezaje kurudi sehemu ambayo sipati maslahi yangu yaliyokuwa kwenye mkataba? na uzuri mkataba unaongea kila kitu hivyo hayo ni matatizo ya hiyo timu sio mimi,” anasema Kapombe.
“Matatizo yaliyotokea kule ni mambo ya mshahara, lakini mimi Kapombe nacheza mpira kama kama kazi kwani kuna watu nyuma yangu wananiangalia, familia yangu yote inaniangalia mimi ndio maana nilienda AS Cannes kwa lengo la kuisaidia familia yangu, nisingeweza kuvumilia kuishi bila mshahara nikaamua kurudi nyumbani na kujiunga na Azam,”anasema Kapombe.
No comments:
Post a Comment