KAMA ilivyo hulka ya binadamu wengi, si rahisi kukubali jambo au kitu kipya hata kama jambo hilo litakuwa na manufaa kwake na kwa jamii iliyomzunguka.
Karne nyingi zilizopita, mmea usiopendeza wa nyanya ulimea katika maeneo ya Andes ya Bara la Amerika ya Kusini, lakini wenyeji wa maeneo hayo Wahindi Wekundu hawakuupanda mmea huo na hata matunda yake.
Mmea huo ulipelekwa nchini Mexico, ambako Waaziteki waliuita “Xitomati” yaani “Tomati” kubwa.
Neno tomati lilitumiwa kwa ajili ya matunda kadhaa yanayofanana na nyanya, hasa matunda yenye umajimaji mwingi.
Muda mfupi baada yam mea huo kupelekwa Maxico, Waaziteki wakaanza kutumia matunda yake katika mchuzi au rojo ya nyanya kwenye mapishi yao. Hatimaye pole pole mmea huo ukaanza kujulikana ulimwenguni pote.
Mwaka 1590, Kasisi wa Kikatoliki wa Shirika la Jeisut aliyeishi nchini Mexico kwa miaka mingi alilisifu tunda la nyanya na kulitaja kama tunda lenye lishe bora na virutubisho.
Jamii ya Wahispania walioishi Mexico, walituma mbegu za mmea huo nchini kwao na pia katika makoloni yao huko Ufilipino na Karrebian.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizo zote, ilichukua zaidi ya karne tatu kabla ya nyanya kuanza kutumiwa katika mapishi uliwenguni kote.
Maoni yasiyofaa
Licha ya sifa ya nyanya nchini Maxico, tunda hilo lilichukiwa sana Ulaya. Tatizo lilianza pale wataalam wa mimea huko Ulaya walipoorodhesha nyanya katika jamii ya “Solanaceae” yaani wakiumanisha mmea huo na jamii moja ya mmea unaojulikana kama Mbeladona wenye sumu.
Mbali na mtazamo huo, wataalam wa mimea, walieleza tunda la nyanya lilikuwa na nguvu ya kuamsha tamaa ya ngono. Watu wengine huamini kwamba hiyo ndiyo sababu Wafaransa waliliita tunda hilo Pomme de” Amour, yaani “Tofaa la Mapenzi”.
Maoni yasiyofaa kuhusu nyanya yalienea hadi Amerika Kaskazini, kwani mwishoni mwa miaka ya 1820, mkulima mmoja Mmarekani kutoka Masschusetts, alikaririwa akisema kuhusu: (Nyanya): “Nilifikiri ningezila tu pindi ninapokuwa na njaa kali sana”.
Mwanaume mmoja kutoka Pennsylvania aliita nyanya kuwa ni “Takataka chungu “. Naye mkulima wa Kiingereza, alitaja tunda hilo kuwa ni “Tofaa la dhahabu linalonuka”.
Hata hivyo, katika karne ya 16 Waitaliano waliliita tunda hilo ‘Pomodoro’, yaani “ Tofaa la Dhahabu”. Inasemekana nyanya zilipewa jina hilo kwa sababu aina za kwanza za nyanya zilizopandwa na Waitaliano zilikuwa na rangi ya njano.
Kutopendwa hadi kupendwa
Watu walipoanza kula nyanya, mashaka waliyokuwa nayo awali yalitoweka, na ukuzaji wa zao la nyanya ukaanza kustawi.
Hadi kufikia miaka ya 1870, kwa kutumia njia ya usafiri wa reli, nyanya zilisafirishwa kutoka Calfornia na kuuzwa New York, Marekani.
Miaka michache kabla ya wakati huo, pahala pa kwanza pa kutengenezea Piza palifunguliwa huko Naples nchini Italia, hivyo kukawa na mahitaji makubwa ya nyanya.
Ukweli kuhusu nyanya
Kila mwaka karibia tani milioni100 za nyanya huvunwa ulimwenguni. Idadi hiyo ni kubwa zaidi ya matunda mengine makuu ulimwenguni kama vile Matofaa, Ndizi, Zabibu na Machungwa.
Ingawa imezoeleka nyanya ni sehemu ya kiungo katika mboga mbalimbali, kulingana na elimu ya mimea nyanya ni tunda.
Hii inatokan na kuwa sehemu yenye mbegu ndiyo inayoliwa (kwa kawaida sehemu za mboga zinazoliwa ni shina, majani, na mizizi).
Kwa mujibu wa kitabu cha The Guinness Book of The Records, tunda kubwa zaidi la nyanya kuwahi kurekodiwa lilipandwa na lilipovunwa huko Oklahama, Marekani lilikuwa na uzito wa kilo 3.5.
Jambo muhimu linalopashwa kuzingatiwa katika kilimo cha nyanya ni kutokuvuta sigara karibu na mimea ya nyanya au kuishika baada ya kuvuta sigara, kwani kuna uwezekano wa mmea huo kudhurika. Sigara ina virusi ambavyo huathiri mmea wa nyanya.
Faida zinazopatikana kwenye nyanya ni nyingi. Mbali na kuwa na Vitamini A na C , ina rangi ya asili inayoitwa lycopene ambayo huzuia kuharibiwa kwa chembe kwa sababu ya hewa ya Oksijeni nyingi.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha chakula kilichopikwa au rojo na mchuzi wa nyanya nyingi kinaweza kupunguza hatari ya kupata Kansa.
No comments:
Post a Comment