Tuesday, 1 July 2014

BRAZIL 2014: AFRIKA HOI

<
Mshambuliaji wa Ujerumani, Andre Schuerrle (kushoto) akifunga bao la kwanza kwa timu yake huku kipa wa Algeria, Rais Mbohli akiruka bila mafanikio akitazamwa na beki wake,  Faouzi Ghoulam, katika mchezo wa jana wa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia uliopigwa kwenye Uwanja wa Beira-Rio, mjini Porto Alegre, Brazil. Algeria ilichapwa 2-1 na kuwa timu ya mwisho kutoka Afrika kutolewa katika fainali hizo.  Picha na AFP 
 Wawakilishi wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia waliokuwa wamebaki, Nigeria na Algeria nao wametolewa katika mashindano hayo.
Katika mchezo wa mapema jana, Nigeria ilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa, yakifungwa na Paul Pogba na beki Joseph Yobo akijifunga.
Algeria walifanikiwa kwenda suluhu dakika 90, lakini dakika 30 za nyongeza zilikuwa mbaya kwao baada ya kukubali mabao 2-1.
Andre Schurrle alifunga dakika ya pili ya muda wa nyongeza kabla ya Metsuit Ozil kufunga la pili, lakini bao la kufutia machozi la Djabou halikutosha kuwaokoa Algeria katika kipigo.
 Wakati hali ikiwa hivyo kwa Waafrika, Uswisi wana kazi ya ziada kuhakikisha inatinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, wakati watakapovaana na Argentina leo.
Kikosi cha kocha Alejandro Sabella kilifuzu kwa hatua ya mtoano kutoka Kundi F wakiwa mabingwa kwa kushinda michezo yote mitatu, ambapo walizichakaza timu za Bosnia-Herzegovina, Iran na Nigeria.
Hata hivyo, Uswisi nayo ilifanya vizuri ilipoishinda Ecuador katika nafasi ya pili ya Kundi E, wakipata nafasi ya kutinga katika hatua ya timu 16 kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Honduras katika mchezo wao wa mwisho wa makundi.
Argentina huenda wakamuanzisha Ezequiel Lavezzi kama winga na hiyo ni kutokana na kuumia kwa nyota huyo wa Manchester City, Sergio Aguero.
Wasiwasi mkubwa kwa Uswisi ni jinsi ya kumzuia Lionel Messi na kazi hiyo inaonekana kukabidhiwa kwa Fabian Schar, ambaye alijihakikishia nafasi baada ya Philippe Senderos katika mchezo dhidi ya Honduras.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!