Friday, 25 July 2014

BOTI ISIYOTUMIA NAHODHA YAVUMBULIWA TANZANIA


Mvumbuzi wa boti isiyotumia nahodha, Emmanuel Bukuku akitoa ufafanuzi wakati wa Maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

 Dar es Salaam. Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta) imevumbua boti inayojiendesha bila nahodha ambayo ina uwezo wa kutuma taarifa za kijasusi na kujilinda dhidi ya mashambulizi au uharibifu unaoweza kufanywa na watu wenye nia mbaya.

Akizungumza wakati wa Maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini hapa jana, Mvumbuzi wa mashine hiyo, Immanuel Bukuku alisema kuwa imemchukua miezi sita kufanikisha uundaji wa mashine hiyo.

Alisema uvumbuzi huo umeambatana na majaribio ambayo yamefanyika katika Pwani ya Kigamboni na yameonyesha mafanikio makubwa na ipo tayari kwa ajili ya matumizi ikiwa na kamera za kutosha kwa ajili ya uchunguzi na kupeleka taarifa.

“Uvumbuzi umekamilika na boti ipo tayari kwa ajili ya matumizi na wadau wanakaribishwa kwa ajili ya kusaidia ufanikishaji wa utengenezaji wa boti nyingine zaidi,” alisema na kuongeza kuwa boti hiyo itakuwa inaongozwa na mashine nyingine itakayo kuwa sehemu maalumu.

Bukuku ambaye ni mwalimu wa masuala ya Sayansi na Teknolojia katika Chuo cha Veta Chang’ombe alisema amevumbua boti hiyo ambayo imetengenezwa kwa kutumia vifaa rafiki na mazingira ya bahari na inatumia mfumo wa umeme jua na mashine za kuzalisha umeme.

“Ina uwezo wa kuhisi kuwapo kwa mtu au chombo kingine jirani yake na kutoa taarifa katika sehemu ambako kinaratibiwa, pia ina uwezo wa kushambulia kwa kutumia mitutu na ina uwezo mkubwa katika masuala ya ulinzi na usalama,” alisema.

Alisema pia amefanikiwa kutengeneza injini ya ndege ambayo imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa na wakati wowote inaweza kutumika na mafanikio hayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mpango wa Veta wa kuwa na Kitengo cha Masuala ya Ufundi na Ubunifu.

“Kuna mashine na teknolojia nyingi ambazo zimevumbuliwa hapa, ni dalili njema na tuna matumaini kuwa uvumbuzi zaidi unafuata kutokana na tafiti nyingi kuonyesha dalili za mafanikio,” alisema na kuongeza kuwa kitengo hicho kimepania kubadili mwelekeo mzima wa Veta kwa hivi sasa.


Chanzo: Mwananchi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!