Pages

Monday, 28 July 2014

ASKOFU ATAKA USHAURI WA RAIS UHESHIMIWE


Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Dodoma, Mhashamu Mathias Isuja

WATANZANIA wameshauriwa kuendelea kuheshimu hadhi na mamlaka aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania, Jakaya Kikwete, kwa kuthamini na kuzingatia mwongozo na ushauri mbalimbali anaoutoa kwa wananchi, kwani mamlaka hayo yanatoka kwa Mungu.



Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Dodoma, Mhashamu Mathias Isuja, amesema hayo jana katika mahubiri yake maalumu wakati wa Misa ya Jumapili katika Parokia ya Makole, Jimbo Katoliki la Dodoma. Misa hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiaskofu Jimbo la Kondoa.
Askofu Isuja, ambaye ni Askofu wa kwanza Mtanzania katika jimbo hilo, aliwataka Watanzania waombe Mungu, ili ajalie busara na hekima katika kutenda na kuamua mambo mbalimbali yahusuyo nchi, hasa kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya.
Alisema hafurahishwi na jinsi makundi mbalimbali ya Watanzania wanavyolumbana na kubeza hata miongozo inayotolewa na Rais Kikwete.
“Imekuwa ni tabia kwa Watanzania kubeza na kudharau ushauri wake pasipo kujua kuwa yeye ameteuliwa na Mungu kuwaongoza Watanzania,” alisema Askofu Isuja.
Alisema ili nchi iwe na amani na upendo bila kugombana, hakuna budi kuitegemea sana busara na hekima ya Mungu, ili kusiwe na kutumbukia katika mizozo itakayohatarisha amani.
Ushauri wa Kikwete
Ushauri wa Rais Kikwete alioutoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, ambao umekuwa ukibezwa na Ukawa, ulihusu maoni yake kuhusu hatari ya muundo wa Muungano wa serikali tatu, unaopendekezwa katika Rasimu ya Katiba mpya, kwa Tanzania na Watanzania.
Katika ushauri huo, Rais Kikwete alinukuu Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya, ambayo pamoja na kupendekeza muundo huo wa serikali tatu, ilieleza wazi athari zake kuwa ni pamoja na kuibuka kwa misuguano na mikwamo katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano.
Athari ya pili ya muundo huo ambayo Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilieleza na ambayo Rais Kikwete aliinukuu, ni kuibuka kwa hisia za utaifa wa zamani kwa nchi washirika.
“Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. “Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia,” alisema Rais Kikwete.
Kukwama uamuzi
Rais Kikwete aliwashauri wajumbe hao kuwa ni lazima lifanyike kila linalowezekana, kuhakikisha kuwa uamuzi wakati wa uendeshaji wa serikali hizo, haukwami kwani ukikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama.
“Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi, Muungano unaweza kuvunjika,” aliasa Rais Kikwete.
Hisia za utaifa
Akizungumzia hatari ya Serikali tatu, ya kuibua na kukuza hisia za utaifa kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari, Rais Kikwete alisema hatari hiyo ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano.
“Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kindugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanzania,” alisema.
Alikumbusha kuwa sensa iliyopita ya 2012, imebaini kuwa takribani asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa, wamezaliwa baada ya mwaka 1964 na nchi wanayoijua ni Tanzania.
Wageni wapya
Rais Kikwete alionya kuwa litakuwa ni jambo lenye mshituko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika, ikiwa watu hao watajikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalumu wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili.
“Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata. Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara moja watajikuta maadui. “Aidha watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma maishani,” aliasa Rais Kikwete.
Alionya kuwa changamoto hizo kubwa mbili za mfumo wa serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli na si mambo ya kufikirika.
Chokochoko
“Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo.
“Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya serikali zetu mbili na kufikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?” Alihoji.
Kutokana na hoja na ushauri huo wenye maonyo, Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa dhamana waliyopewa ya kuamua kwa niaba ya wananchi, kupima mambo hayo kwa umakini mkubwa ili wafanye uamuzi ulio sahihi.
“Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika, halitakuwa jambo la ajabu. Kwa kweli unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi waliamua walivyoamua. “Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo,” alisema.
Pia alikumbushia ushauri uliowahi kutolewa na kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini, ambaye Rais Kikwete alisema kiongozi huyo alimuuliza: “Hivi Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu, si kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili. Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi.”
Kutokana na ushauri huo wa kiongozi wa kidini, Rais Kikwete alisema pengine na ushauri huo wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Ushauri Ukawa
Baada ya kuwataka Watanzania kutilia maanani ushauri wa Rais kutokana na nguvu ya ushauri wake inayotoka kwa Mungu, Askofu Isuja pia aliasa kundi la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa kuwataka kujipima kama wanatumia hekima katika kujadili na kuwapatia Watanzania Katiba mpya.
Alisema kutofautiana kifikra si kosa, ila pawepo na busara katika kuridhiana na kufikia hitimisho ambalo matokeo yake ni kuleta amani, umoja na ustahimilivu kwa Watanzania wote na si kama inavyoonekana hivi sasa.
Askofu Isuja alisema yeye ni Mtanzania na mtumishi wa watu, hivyo analojukumu la kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa kitu kimoja, wakisaidiana, kuheshimiana na kuvumiliana haswa pale panapotakiwa jambo la pamoja kama Watanzania.
Aliwataka viongozi wa kada mbalimbali hapa nchini, kuomba busara kutoka kwa Mungu, kama alivyofanya Suleimani aliyekuwa Mfalme wa Israel, ambaye alipopewa ufalme na Mungu, kitu cha kwanza alimwomba Mungu ampatie hekima ya kuamua mambo yote kwa haki.
Alisema, Watanzania ni wengi kiasi ambacho ni vigumu kwa kiongozi moja kutenda kwa usahihi hadi watu wote waridhike. “Suleimani alilitambua hilo, na akaomba hekima ya Mungu ili imwongoze kutenda kwa haki na kuamua kwa hekima,” alisema.

No comments:

Post a Comment