Saturday, 12 July 2014
ALIYEKUFA NA MGANGA WA JADI SHIMONI BAADA YA KUKOSA HEWA AZIKWA HUMO HUMO!
KIKOSI cha uokoaji kimeshindwa kuupata mwili wa Zuberi Kaima (45) ambaye yeye pamoja na mganga wa jadi, Sophiani Khamis (60) walisadikiwa kufa kwa kukosa hewa kwenye shimo walilokuwa wakichimba dhahabu.
Kaimu Kamanda wa kikosi cha Uokoaji, Augustino Magere alisema juzi kuwa juhudi za kuutoa mwili wa marehemu huyo hazikufanikiwa kutokana na kuwepo ufinyu wa nafasi ndani ya shimo hilo hivyo kushindwa kumfikia.
Alisema pia kutokuwepo kwa hewa ya kutosha iliyosababisha vifo vya watu hao na hivyo kuhofia kusababisha madhara mengine yasiyotarajiwa kwa waopoaji.
Hata hivyo mwili wa marehemu mganga wa jadi, Sophian Hamisi aliyeoteshwa kuwepo kwa dhahabu katika eneo la Kangaye ‘A’ na kusababisha maafa hayo kwa kukosa hewa umezikwa juzi mchana kwenye makaburi ya Kangaye ‘ A’ wilaya ya Ilemela.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Amina Masenza juzi alifika katika eneo la tukio ambako mwili wa marehemu Zuberi ulishindikana kuopolewa na kuwataka wanafamilia wafanye maridhiano ya maziko na kitakachokubalika kifanyike.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limethibitisha maziko hayo ambayo yamefanyika kwenye miamba ya shimo hilo baada ya kukosekana nafasi ya kuuopoa mwili huo na pia kuogopa kusababisha madhara mengine kwa askari waliojaribu kuopoa mwili uliobakia shimoni.
Eneo hilo la Kangaye ‘A’ linalosadikika kuwa na dhahabu lilizuiliwa kuchimbwa baada ya kubainika kwamba linahatarisha maisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment