“Kwa miaka minne mfululizo maelfu ya tani za mkaa wa mawe yamekuwa yanasombwa na maji kutoka katika Kijiji cha Ndumbi hadi ndani ya Ziwa Nyasa, wananchi wanatumia maji hayo kwa ajili ya kunywa,’’ anasema Mwenyekiti wa kijiji hicho wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, James Mbawala.
Anasema Kampuni ya Mkaa wa Mawe ya TANCOAL ambayo inachimba mkaa wa mawe katika eneo la Ngaka wilayani Mbinga ndiyo inayoitumia Bandari ya Ndumbi, Ziwa Nyasa kwa ajili ya kusafirishia mkaa wa mawe kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Mbawala anasema katika bandari ya kijiji hapo ni mahali pa kupitishia mkaa huo na kwamba kijiji hicho hakina huduma ya maji ya bomba badala yake wananchi wanatumia maji ya Ziwa Nyasa kwa maji ya kunywa na matumizi mbalimbali.
Ushirikishwaji katika EIA
Kwa kawaida Serikali inapokusudia kuanzisha miradi mikubwa kama ya madini, katika tathmini ya mazingira yaani Environmental Impact Assessment (EIA) inatakiwa Serikali kuwashirikisha wananchi katika eneo husika ili kubaini iwapo mradi huo utakuwa na madhara au laa, mwenyekiti huyo anadai kuwa Serikali haikuwashirikisha ilipoamua kuitumia Bandari ya Ndumbi kwa ajili ya kusafirishia mkaa wakati wa utafiti na sasa wakati wa uchimbaji na uuzaji.
Sera ya mazingira ya mwaka 1997 ambayo imetumika kutunga sheria mama ya mazingira ya mwaka 2004 katika kifungu cha 4 (1) na kifungu cha 5 (1) inaeleza wazi kuwa kila mtu Tanzania ana haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na afya njema hivyo hatua za uchimbaji wa madini iwapo siyo salama inaweza kutumika sheria hii kudai haki.
Mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa Lawyers Environmental Action Team (LEAT), Dk Nshala Rugemeleza anasema sheria mama ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 21 inaonyesha wazi miradi yote mikubwa inayotakiwa kufanyiwa tathmini ya mazingira (EIA) miradi ambayo inabadilisha asili ya umbile la eneo husika kama ilivyo kwa mkaa wa mawe ambao umebadilisha asili ya umbile la Bandari ya Ndumbi.
Dk Nshala anasisitiza kuwa iwapo taratibu za EIA hazikufuatwa wadau wanaweza kupeleka malalamiko yao mahakamani ili kudai haki pia mwekezaji anatakiwa kurudishia mazingira aliyoyaharibu katika Bandari ya Ndumbi baada ya mradi kwa kuyarekebisha ili kurejea katika hali yake ya asili kabla hajaondoka. Kulingana na Dk Nshala mfumo wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta ni mbovu, hivyo uangaliwe
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment