Wednesday, 25 June 2014

WALIOMUUA SISTA WASAKWA KILA KONA



POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeanzisha msako mkali, kuwatafuta watu waliohusika na mauaji ya Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka jijini Dar es Salaam, Sista Cresencia Kapuri (50), ambao utahusisha vikosi vyote vya Polisi. Vikosi hivyo ni Usalama Barabarani, askari wa doria wanaotumia pikipiki na magari, wapelelezi na askari Polisi wa kawaida.


Mauaji ya mtawa huyo, yalitokea juzi mchana katika eneo la Ubungo Riverside, jijini humo, ambapo alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kumpora Sh milioni 20 pamoja na nyaraka mbalimbali za ofisi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari ofisi kwake jana kuwa Sista Cresencia wakati anapigwa risasi, alikuwa ameongozana na wenzake, ambao ni Sista Brigita Mbaga (32) na dereva wao Mark Mwarabu, aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up, yenye namba T213 CJZ.
Kova alisema wakati watawa hao, wakitoka katika Benki ya CRDB Tawi la Mlimani City, walipofika Ubungo Riverside kulipa deni la chakula katika duka la Thomas Francis, ndipo walitokea watu hao wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa na pikipiki, ambayo haikusomeka namba, huku mmoja akiwa na bunduki aina ya SMG.
“Yule dereva wa gari la masista walimpiga risasi katika kidole gumba cha mkono wa kulia na kisha kumpiga mtawa huyo risasi ya kifuani na kupora kiasi hicho cha fedha na nyaraka hizo,” alisema Kova.
Alisema kuwa jambo kubwa walilogundua ni kuwa matukio mengi ya ujambazi, hasa unaohusisha wananchi kuporwa kiasi kikubwa cha fedha, yanaanzia katika mabenki, hivyo kuna uwezekano wa watu ambao si waaminifu, wanafanya uhalifu huo.
Alisema kuwa katika matukio ya aina hiyo, majambazi huwafuatilia wateja wanapoingia au kutoka katika benki mbalimbali.
Alisema imeonekana kwamba mara nyingi benki, zinapohitaji kusafirisha pesa nyingi, hutumia askari au taasisi nyingine za usalama kusafirisha fedha zao.
“Tunawaomba mameneja wa benki zote, kuhakikisha yanawahimiza wateja wake kutumia njia mbadala za kusafirisha pesa nyingi, kama vile matumizi ya hundi, kufanya miamala bila kadi, matumizi ya kadi za kutolea fedha (ATM) na njia nyingine ambazo ni salama.
“Matukio kama haya, yanaonesha ni wazi huu utaratibu wa watu kutoa pesa nyingi kutoka benki na kwenda kufanya malipo si salama. Kuna baadhi ya huduma, kwa mfano kuna baadhi ya nchi ambazo ni sheria mtu haruhusiwi kutembea na fedha nyingi, kwa hiyo ni muhimu kwa sisi wenyewe tukajielewa kwanza,” alisema Kova.
Alisema pia wanaomba mameneja wa benki, kuhakikisha benki zao zinakuwa na kitengo maalumu cha ushauri wa masuala ya usalama kwa wateja wao.
Alifafanua kuwa kama mteja atafika katika benki zao na akahitaji kutoa fedha nyingi ni vyema wakamshauri ;na kama atakaidi, benki ichukue hatua ya kutaarifu Polisi.
Aidha, alitaka wafanyabiashara na taasisi mbalimbali, zisitumie njia za mkato katika usafirishaji na uhifadhi wa pesa zao kwa faida ya usalama wa maisha na mali zao.
Aidha, Kova alisema katika kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo wa kutumia pikipiki, wamezikamata pikipiki 668, ambazo wanazitilia shaka na wanazifanyia ukaguzi zaidi. Pia, zipo ambazo zimekamatwa kuhusiana na makosa mengine ya barabarani

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!