Wednesday, 4 June 2014

UTAFITI WABAINI MILIMA YA SAMUNGE IMEJAA DHAHABU

 
Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini, Kanda ya Kaskazini wamethibitisha uwepo wa hazina ya madini ya dhahabu katika Mlima Rankiroga na Mto Karabaline katika Kijiji cha Mgongo, Kata ya Samunge, Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane alisema jana kuwa Ofisi yake imefanya utafiti wa awali katika Kijiji cha Mgongo na kubaini uwepo wa dhahabu hiyo.
Wamiminika
Gazeti hili lilikuwa la kwanza kuripoti uwepo wa dhahabu hiyo baada ya maelfu ya watu kumiminika tena katika eneo la Samunge, lililokuwa maarufu baada ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile kutangaza kuwa na dawa inayonywewa kwa kikombe kutibu maradhi sugu.
Habari kutoka Samunge zinasema wachimbaji wanazidi kumiminika kusaka madini hayo yaliyogundulika kuwapo kwenye mashamba ya watu na maeneo ya kingo za mto huko Mgongo, kijiji kilichopo jirani na kwa Mchungaji Mwasapile, maarufu kama Babu wa Loliondo.
Diwani wa Samunge, Jackson Sandea alisema maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefurika katika kijiji hicho... “Hadi sasa kuna watu zaidi ya 4,000 na bado wanaongezeka. Hii inaweza kuwa ni zaidi ya kipindi kile cha Babu. Dhahabu hii inapatikana mtoni tu. Watu wanakusanya michanga na kupata dhahabu, hakuna mtu ambaye anachimba.”
Alisema tofauti na maeneo mengine, dhahabu ya Samunge inaonekana ni ya Watanzania wote kwani ipo eneo la mto ambao unamilikiwa na Serikali na ndiyo sababu watu wanaingia kwa wingi. “Kuna wengine wanapata (dhahabu), hata mashambani lakini mtoni ndipo inapatikana kwa wingi zaidi.”
Matokeo ya utafiti
“Ni kweli kuna dhahabu katika eneo la Mto Karabaline na kiasi kikubwa kipo katika eneo la Mlima Rankiroga,” alisema Magayane. Mlima huo upo jirani na Mto Karabaline ambako dhahabu ilianza kugundulika. Wachimbaji wamekuwa wakiomba idhini ya Serikali kuchimba dhahabu katika mlima huo.
Magayane aliwataja wataalamu waliofanya utafiti huo kuwa ni Mtaalamu wa Miamba, Fatuma Kijanda; Fundi Sanifu Mkuu, Zephelin Kalunde na Fundi Sanifu Mwandamizi, Aloyce Mlaga.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kujua ujazo wa dhahabu katika eneo hilo na muda ambao uchimbaji unaweza kuchukua... “Tumepeleka baadhi ya miamba katika ofisi za uchunguzi Dodoma na tunatarajia kupata taarifa karibuni.”
Hata hivyo, alisema dhahabu inayopatikana kwenye Mto Karabaline inaweza kumalizika ndani ya miaka miwili tofauti na ile ya mlimani ambayo alidokeza kuwa itachukua muda kuisha
Wajitokeza kuomba vitalu
Magayane alisema kutokana na kuthibitika uwepo wa dhahabu katika eneo hilo ofisi yake imepokea maombi 14 ya kuchimba.
Alisema walioomba wote ni Watanzania na hakuna kampuni ya kutoka nje ya nchi.
Kuhusu taratibu za utoaji wa leseni alisema: “Nitakwenda Ngorongoro hivi karibuni na kuonana na viongozi wa Serikali kwanza kujua umiliki wa ardhi hiyo kabla ya kutoa leseni.”
Taarifa hiyo ya wataalamu wa Serikali imetolewa takriban miezi matatu tangu wachimbaji wadogo walipogundua madini hayo huku Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali akipinga taarifa za uwepo wa madini hayo.
Lali ambaye alikuwa hajafika Samunge tangu uchimbaji ulipoanza wiki iliyopita, aliibuka na kupinga taarifa za watu kuongezeka Samunge kuchimba dhahabu

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!