Sunday, 22 June 2014

TMAA YAOKOA BILIONI 15 ZA MADINI, YAPONGEZWA


????????Mashine ya kisasa ya kupimia ubora wa sampuli za madini ikioneshwa kwenye Banda la TMAA wakati wa Maadhimisho ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.????????Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hab Mkwizu (Kushoto) akizungumza na watumishi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) alipowatembelea kwenye Banda lao. Wanaomsikiliza ni Afisa Habari, Mhandisi Yesambi Shiwa (Kulia) na Afisa Utumishi, Bibi Fatma Chondo (Katikati).????????Makaa ya mawe yakioneshwa kwenye Banda la TMAA wakati wa Maadhimisho ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………..
Na Saidi Mkabakuli
Serikali imeupongeza Wakala wa ukaguzi wa madini nchini (TMAA) kwa kufanikiwa kuokoa kiasi kikubwa cha madini yaliyokuwa yakitoroshwa kinyemela katika viwanja vya ndege nchini hivyo kuokoa zaidi ya bilioni 15 zilizolipwa kama mrahaba tangu ilipoanzisha ukaguzi maalum kwa wasafiri waendao nje ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hab Mkwizu alipokuwa akikagua utendaji kazi wa Wakala katika maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Bw. Mkwizu alisema kuwa kwa muda mrefu sasa wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiitia hasara Serikali kwa kukwepa ulipaji wa kodi wa madini yaendayo nje ya Tanzania kinyume na utaratibu uliowekwa.
“Hongereni sana kwa kuweza kuokoa kiasi kikubwa cha madini yaliyokuwa yakisafirishwa bila kufuata taratibu zetu za usafirishaji wa madini yaendayo nje ya Tanzania,” alisema Bw. Mkwizu.
Naibu Katibu Mkuu Mkwizu aliwasihi viongozi na watumishi wa Wakala kuongeza uchapaji kazi na uzalendo ili kuweza kukomesha kabisa tabia ya wafanyabiashara hao wasio waaminifu.
Akikaribishwa kwenye banda la Wakala kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja na Afisa Habari wa Wakala hiyo, Mhandisi Yisambi Shiwa, Bw. Mkwizu alijulishwa kuwa moja kati ya mafanikio yaliyofikiwa na Wakala mara baada ya ukaguzi wa ziada kwa wasafiri waendao nje ya Tanzania, ni pamoja na kubainika mamia ya wafanyabiashara wa madini ambao wamekuwa wakitorosha kinyemela madini ya thamani kubwa ya fedha bila kufuata taratibu.
“Katika kuboresha utendaji kazi wa Wakala, tulitambulisha mpangokazi mpya wa ukaguzi wa ziada katika viwanja vyetu vya ndege vikubwa vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na kile cha Mwanza lengo ni kubaini wafanyabiashara wasio waaminifu na ndipo tulipobaini wizi huu,” alisema Mhandisi Shiwa.
Akizungumzia thamani ya madini hayo, Mhandisi Shiwa alisema kuwa kufuatia ukaguzi huu, mpaka sasa Wakala imeweza kuokoa madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 15.
“Ukaguzi huu umesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha madini yenye thamani ya shilingi bilioni 15.3 hadi kufikia mwaka na hivyo kuiongezea serikali yetu mapato ambayo yalikuwa yatoroshwe na wafanyabiashara hao wasio waaminifu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mhandisi Shiwa, kiasi hiki cha fedha ni sehemu ya mrahaba wa kisheria unaostahili kuchangiwa na wafanyabiashara hao kwa umiliki wao wa madini hayo kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Mhandisi Shiwa aliongeza kuwa katika kuendelea kudhibiti tabia hizi, Wakala kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali imekuwa ikishikilia na kutaifisha madini yanayotiliwa shaka ama kumilikiwa isivyo halali yanayopatikana katika viwanja hivyo.
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa tarehe 2 Novemba, 2009 chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245. Tamko la Waziri la kuanzisha Wakala lilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 362 la tarehe 6 Novemba, 2009.
Lengo la Wakala ni kuhakikisha kwamba, Serikali inapata mapato stahiki kutoka kwenye shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini kupitia usimamizi na ukaguzi makini wa shughuli za uchimbaji, na kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji thabiti wa mazingira katika maeneo ya migodi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!