Thursday, 12 June 2014

SHILINGI YAENDELEA KUPOROMOKA

Kwa wananchi wa kawaida au wafanyabishara wadogo wasionunua au kuuza bidhaa zao nje ya nchi, huenda wasifahamu kiundani kinachoendelea kuhusu thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Wengi hawafahamu kuwa kwa takriban wiki tisa mfululizo fedha yao, ambayo pia na utambulisho wa nchi, imeshuka thamani kwa kiasi kikubwa dhidi ya Dola ya Marekani.
Kwa sasa wastani wa kununua dola moja katika benki za biashara na baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha, ni kati ya Sh1,690 hadi 1,700 wakati kiwango cha kuuza ni Sh1,680.
Kiwango hicho ni kikubwa zaidi takriban ongezeko la Sh50 kwa kila Dola kuliko kile kilichokuwepo miezi mitatu iliyopita. Na kwa hali ilivyo ufanisi wa shilingi na hata uchumi wa nchi vinaweza kuwa shakani.
Chanzo cha tatizo
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanabainisha sababu kuu mbili zilizochangia kushuka kwa shilingi na kubaki katika hali hiyo kwa wiki tisa mfululizo.
Sababu ya kwanza wanataja kuwa ni kitendo cha serikali kuruhusu matumizi ya dola hiyo katika malipo halali ya ndani, hivyo kutengeneza mahitaji makubwa ya fedha hiyo yenye nguvu kubwa duniani.
Pia wanasema kuwa hali hiyo ni matokeo ya kutouza bidhaa au huduma nyingi nje ya nchi, hivyo kusababisha ukame wa dola ambayo kwa asilimia kubwa hupatikana kupitia njia ya biashara za kimataifa.
“Hali hii inamaanisha Tanzania tunanunua bidhaa nyingi sana nje ya nchi kwa kutumia Dola ya Kimarekani kuliko kile tunachouza kwa nchi hizo,’’ anasema mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Wineaster Anderson.
“Sekta nyingi muhimu nchini kama viwanda, madini, usafirishaji na kilimo zinaagiza bidhaa nje ya nchi katika kujiendesha, hivyo kutengeneza mazingira ya Dola kuadimika na kupanda thamani.”
Anaeleza kuwa hata uuzaji bidhaa za kilimo na madini, ambazo Tanzania hutegemea kuziuza nje, haufanyi vizuri tofauti na kipindi cha nyuma jambo linalopunguza upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.
Kauli ya Dk Anderson juu ya kupungua kwa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, inakwenda sambamba na ripoti ya Benki Kuu ya Aprili 2014 kuhusu mwenendo wa uchumi nchini
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kwa mwaka ulioishia Machi 2014, thamani ya uuzaji bidhaa nje ya nchi ilipungua kwa asilimia 1.7 na kuleta mapato ya Dola 8,709.5 milioni za Kimarekani tofauti na ilivyokuwa mwaka mmoja nyuma.
Inaongeza kuwa katika kipindi hicho, bidhaa za viwandani na usafirishaji pekee ndizo zilizofanya vizuri.
Kwa mfano, dhahabu, ambayo imebaki kuwa mhimili wa uuzaji bidhaa nje ya nchi, ilishuka na kuingiza kiasi cha takriban Dola 1.75 bilioni za Kimarekani kutoka 1.97 bilioni mwaka 2013.
Ukitoa kuyumba kwa biashara za kimataifa hususan uuzaji wa bidhaa na huduma, kwa upande wake, Dk Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema suala la Serikali kuruhusu matumizi ya dola katika baadhi ya malipo linazidi kuihatarisha fedha ya Tanzania.
“Hili ni tatizo kwa sababu hawa watoa huduma au wauzaji wa bidhaa, wanauza bidhaa kwa bei ile ile ya dola licha ya kwamba shilingi imeshuka. Hii sasa itafanya watu kuhangaikia kununua dola jambo linaloua fedha yetu,” anaeleza.
Ili kuinusuru shilingi, Dk Ngowi anasema kuna haja ya serikali na wadau kuchochea uuzaji wa bidhaa nje, kukuza sekta ya utalii na kupunguza matumizi ya dola nchini.
Naye mkuu wa idara ya ubadilishaji wa fedha wa benki ya biashara ya FNB, Patrick Kapella anakiri kuwa shilingi haijafanya vizuri zaidi kwa miezi miwili mfululizo, hivyo kuathiri biashara nyingi. “Haya ni mabadiliko makubwa katika mahitaji na upatikanaji wa Dola ndani ya muda mfupi, ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka jana.
“Kwa sasa Dola imeadimika kutoka kwenye sekta za madini na bidhaa za kilimo, huku mahitaji yake kwa ajili ya uingizaji wa bidhaa yakizidi kukua,” anasema.
Kapella anaongeza kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara walijizuia kubadili fedha zao kwenda kwenye Dola kwa takriban mwezi mzima wakiamni itashuka, lakini haikuwezekana.
Hata hivyo, anaamini kuwa hali ya shilingi kushuka thamani haitadumu sana na kwamba itaimarika baada ya kutolewa bajeti kuu ya Serikali inayotarajiwa kuwekwa hadharani leo.
Anasema kwamba kuna baadhi wafanyabiashara wanashindwa kufanya uamuzi wa kibiashara wakisubiri iwapo kuna mabadiliko yoyote ya kisera katika bajeti. Hali ya kupanda kwa Dola si mara ya kwanza kutokea kwani ilishawahi kutokea mwaka 2011 ambapo Dola moja ilikuwa ikibadilishwa kwa kiwango cha kati ya Sh1,800 na kwa mujibu wa Kapella kwa hali ilivyosasa haijafikia hata nusu yake.
Mtazamo huo unaungwa mkono pia na mkurugenzi wa utafiti wa uchumi na sera, Dk Joseph Masawe, ambaye aliliambia gazeti la The Citizen hivi karibuni kuwa Watanzania wasiwe na hofu kwani hilo ni tukio la muda na linalopita
Anasema kuwa wakati shilingi ikishuka thamani kwa asilimia nne kutoka Januari 2012 hadi mwishoni mwa Aprili mwaka huu, Fedha ya Afrika ya Kusini (Rand) ilishuka kwa asilimia 35 hali kadhalika Rupee ya India ilishuka kwa asilimia 21.
Anaongeza kuwa fedha yoyote inayoongozwa na mabadiliko ya soko ni lazima ipate mtikisiko wa muda mfupi hali kadhalika muda mrefu.
Athari kwa Watanzania
Pamoja na kwamba wataalamu wanasema ni hali ya muda mfupi, Watanzania wanazidi kuathirika na kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa na huduma.
“Hali hii inagusa moja kwa moja Watanzania na tayari baadhi ya bidhaa zinazofuata sana muenendo wa Dola zimeshapanda bei.
Iwapo hali itadumu kwa muda mrefu itawaathiri sana wananchi kimaisha,” alisema.
japo ni nina imani kubwa sana kwamba BOT watashuhulikia hili tatizo,” anasema Dk Ngowi.
VIA-MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!