MAHAKAMA nchini Marekani imetoa uamuzi kwamba Mtanzania, Khalfan Khamis Ghailan (40), aliyefungwa kifungo cha maisha kwa mashambulizi dhidi ya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, ana haki ya kuwasiliana na ndugu zake.
Akisoma uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Marcia Krieger alisema marufuku ya mawasiliano aliyowekewa kijana huyo, haikuwa na mashiko ya kisheria na yalikosa ushahidi wa kuithibitisha.
Katika hukumu yake ya kurasa 45, Jaji Krieger alisema hakuridhishwa na ushahidi kutoka Ofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kwamba Khalfan amekuwa akigoma kula, kutoa kauli mbaya dhidi ya Marekani na kuwazulia uongo wafanyakazi wa jela.Jaji huyo aliliamuru Shirika la Upelelezi la FBI na maofisa wa Jela, kupitia upya orodha ya majina ya watu, ambao wanaweza kuwasiliana naye. Kaka wa Khalfan, Rubea Khamis aliyeko Zanzibar alikaririwa akisema:
“Hukumu hii ina maana kubwa kwa familia yetu, ataweza kuzungumza na watoto na jamaa zake ambao wamekuwa wakimjua kupitia hadithi tu."
Ghailan alikuwa ameishitaki FBI na Idara ya Magereza ya nchi hiyo, kwa kumzuia kuwasiliana na ndugu na marafiki zake kadhaa, akiwamo mmoja wa kaka zake, akihoji kwamba marufuku hiyo ni kinyume cha Katiba ya Marekani.
Kijana huyo alitiwa hatiani kwa kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa kundi la al-Qaida na amefungwa kwenye gereza lililopo jimbo la Colorado, linalotajwa kutumika kufunga watu wanaominika kuwa hatari
VIA-HABARI LEO
No comments:
Post a Comment