Vijana wanatajwa kuwa ni chachu ya maendeleo na nguzo kubwa katika mapinduzi ya kiuchumi kwa taifa.
Hata hivyo taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa Mei mwaka huu zinaeleza kuwa vijana wengi wameathirika na hata kupoteza maisha kutokana na msongo wa mawazo.
Magonjwa yasababishwayo na msongo wa mawazo yanayotajwa na WHO ni pamoja na maradhi ya akili, moyo, ugumba, ukosefu wa nguvu za kiume na ulevi kupindukia.
Katika sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, takwimu zilieleza kuwa kati ya Watanzania 10 wanne ni vijana. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 35 au jumla ya watu milioni 16 kati ya watanzania milioni 45.
Utafiti uliofanywa na WHO ulibaini kuwa nusu ya watu wote duniani wanaougua magonjwa ya akili waliyapata wakiwa katika umri wa chini ya miaka 15 kutokana na msongo wa mawazo.
Sababu za msongo wa mawazo
Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo anasema moja ya mambo yanayosababisha vijana kunywa pombe bila utaratibu ni msongo wa mawazo.
Chanzo cha misongo hiyo ya mawazo ni pamoja na kukosa ajira au kutokutimiza malengo yao.
Anasema sigara na pombe ni vitu vinavyopoteza muda na kujisahaulisha matatizo.
Kwa sababu hiyo akaonya kuwa wengi wanakosa kitu cha kufanya na wanachanganyikiwa hivyo wanadhani suluhisho ni moja tu, kunywa pombe.
“Vijana kama hawa hakuna namna ya kuwasaidia, kwa sababu chanzo kikubwa ni ufinyu wa sekta binafsi unaosababisha ukosefu wa ajira,” anasema.
Anasema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vijana wanaotoka vijijini kuja mijini na wote wanatafuta ajira, wanapozikosa basi hujiingiza katika unywaji pombe.
“Ni lazima tuwe wabunifu ili kuwafanya vijana wavutiwe na mazingira ya vijijini. Bila hivyo hakuna atakayekiona kilimo kama ajira bali adhabu na hicho ndicho huwafanya wakimbilie mijini na kuishia kwenye ulevi,” anasema.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Innocent Mosha anasema unywaji wa pombe unasababisha madhara mengi kiafya, ikiwemo saratani ya koo.
“Pombe na sigara ni sababu mojawapo, lakini saratani inasababishwa na mambo mengi,” anasema.
Ingawa kuna sheria ya ununuzi wa pombe inayokata mtu mwenye umri chini ya 18 kununua pombe, sheria hiyo haizingatiwi wala haitekelezwi vijijini ambako kuna wanywaji wengi zaidi.
Anasema vijijini watoto wengi wenye umri wa kuanzia miaka 10 ni wanywaji wa pombe za kienyeji.
Unywaji huo pia anasema unashamiri zaidi vijijini kwa sababu sheria nyingi zinatekelezwa mjini.
Sababu za vifo kwa vijana
Mwaka 2012 vijana milioni 1.3 duniani walifariki kutokana na ajali za barabarani, Ukimwi na wengine kwa kujiua.
Ukimwi ulishika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo kwa vijana duniani, na WHO inaeleza kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na Ukimwi inaongezeka kila siku katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ilibainika kuwa vifo vitokanavyo na Ukimwi vinaongezeka barani Afrika wakati idadi hiyo inapungua katika nchi zilizoendelea.
Utafiti wa WHO uliangalia sababu nyingi za vifo na msongo wa mawazo, ukijumuisha uvutaji wa tumbaku, pombe, dawa za kulevya na Ukimwi.
“Hatutakiwi kuacha juhudi za kuhimiza afya ya uzazi kwa vijana
Magonjwa mengine ya kuambukiza yaliendelea kuongoza kwa kuua licha ya kuwepo kwa juhudi za kimataifa.
WHO ilizitaka nchi wanachama kuangalia kwa umakini magonjwa kama kuhara, matatizo ya mfumo wa hewa ambayo yalishika nafasi ya juu kwa kusababisha vifo kwa vijana.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja anatoa rai kuwa unywaji wa pombe una madhara kiafya jambo ambalo limeifanya wizara hiyo kukataza matumizi yake.
Mwamaja anasema hata hivyo changamoto kubwa inasababishwa na pombe na sigara kutegemewa na Serikali katika kuongeza mapato yake.
Siku za karibuni serikali ilipiga marufuku pombe kali na viroba.
“Suala la matumizi ya pombe halina budi kufuatiliwa kuanzia ngazi ya familia,” anasema
Ripoti ya utafiti wa WHO inaonyesha kuwa ajali za barabarani zinashika nafasi ya pili kwa kusababisha maradhi na ulemavu kwa vijana ambapo vijana wa kiume walionekana kuathirika mara tatu zaidi kuliko wasichana.
Inaelezwa kuwa msongo wa mawazo hausababishwi pia na wazazi au walezi kuwa wakali kupita kiasi, mazingira na hofu ya maradhi wakati wa ukuaji kwa vijana.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment