Tuesday, 24 June 2014

MAMA AMUUA MTOTO WAKE KISA KAKOJOA KITANDANI


Kaka wa marehemu (Munili Omary), Omary akiwa kwenye msiba wa mdogo wake.
Tukio hilo lililoacha simanzi kwa wanafamilia na wakazi wa Kitongoji cha Mpakani lilitokea saa 2 asubuhi ya Juni 18, mwaka huu.

WAKATI wanaharakati wanaendelea kupiga kelele kuhusu kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji kwa watoto duniani kote,  mwanamke aliyetajwa kwa jina la Amina Hamis, mkazi wa Kata ya Kwembe, Malamba Mawili Kitongoji cha Mpakani, Kinondoni jijini Dar ametiwa mbaroni  kwa madai ya kumuua kwa kipigo mtoto Munili Omar (6).

Awali, habari za madai ya mtoto huyo kuuawa yalitua kwenye chumba cha habari cha Uwazi ambapo mwandishi wetu alifunga safari hadi eneo la tukio.
Mtu wa kwanza kuonana  naye alikuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, James Nyanda ambaye alikiri kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili.
Mwanamke aliyetajwa kwa jina la Amina Hamis, mkazi wa Kata ya Kwembe, Malamba Mawili Kitongoji cha Mpakani, Kinondoni jijini Dar anayeshikiliwa kwa kesi ya kumuua mwanaye
MAMA ADAIWA KUYUMBISHA MAELEZO
Akizungumza na gazeti hili kuhusu mkasa mzima wa mtoto huyo, mwenyekiti huyo alisema:
“Ilikuwa saa 2 asubuhi ya Juni 19, nikiwa nyumbani kwangu nilipigiwa simu na msamaria mwema na kunifahamisha kwamba nyumbani kwa Juma Omar kulikuwa na msiba wa kutatanisha uliotokea jana yake, yaani Juni 18 asubuhi.
Baba wa marehemu, Bw. Juma Omar.
“Baada ya kupata taarifa hiyo, saa 3 asubuhi nilikwenda eneo la tukio na kukutana na Amina anayetuhumiwa kufanya mauaji hayo akiwa na baadhi ya ndugu, majirani na wifi yake anaitwa Faudhia Idd. Nilihoji kuhusiana na kifo hicho, wakaniambia mtoto alifariki dunia baada ya kuanguka.
“Niliuliza sababu ya kukaa na maiti hiyo ndani kwa siku nzima bila kuipeleka hospitali, nikajibiwa alikuwa akimsubiri mumewe ambaye hakuwepo.
Shangazi wa marehemu Faudhia Iddi (kulia) akiwa na waombolezaji wengine.
“Niliomba namba za simu za mumewe ili nimjulishe msiba huo, akanipa. Nilimpigia, nikamweleza mwanaye amefariki dunia hivyo arejee nyumbani, akaniambia alikuwa safarini Ilula (Iringa) hivyo mtoto azikwe tu.
“Alipotoa kauli ile nilishangaa sana, nikamwambia arudi nyumbani kwa sababu tusingeweza kumzika mwanaye bila yeye kuwepo, akasema atarudi.”
Bibi wa marehemu (kulia) akiwa na waombolezaji wengine.
POLISI WAPIGIWA SIMU KUJULISHWA
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema: “Kutokana na utata wa kifo hicho niliamua  kuwapigia simu polisi wa Kituo cha Mbezi Kwayusuf ambao walifika, wakamchukua Amina, wifi yake na mwili wa mtoto huyo wakaupelea kuuhifadhi Hospitali ya Tumbi (Kibaha) kisha mama huyo kushikiliwa kituoni kumsubiri mumewe.
“Mume ambaye hakujua kiini cha kifo cha mwanaye alipowasili aliunganishwa na mkewe kituoni lakini polisi walishindwa kuwa na ushahidi wa mtoto huyo kuuawa hivyo waliandika RB ya KIFO CHA UTATA kisha wakaruhusiwa kurudi nyumbani kuandaa taratibu za mazishi ya mtoto wao,” alisema mwenyekiti.
Ustaadhi akiswalia mwili wa marehemu Munili Omary.
AKINA MAMA WA KITONGOJI WAKATAA
Mwenyekiti huyo aliendelea kusimulia kwamba, kufuatia akina mama wa Kitongoji cha Mpakani kutilia shaka kifo cha mtoto huyo waliyedai alikuwa akinyanyaswa na kupigwa mara kwa mara, kurushwa kichura, kufungiwa ndani, kunyimwa chakula, kukataa kumpeleka hospitali kwa madai angelazwa jambo ambalo hakuhitaji kulisikia, waliamua kumbana wifi yake Faudhia, ndipo akaweka wazi kwamba kifo chake kilitokana na kipigo!!!
Kwa mujibu wa maelezo ya Faudhia, siku ya tukio, marehemu Munili ambaye mama yake mzazi anaishi Nzega, Tabora, alikojoa kitandani ndipo mtuhumiwa akampeleka sebuleni na kuanza kumchapa mwilini na kichwani hadi akakata roho mbele yake.
Waombolezaji wakiuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya maziko.
FAUDHIA ALIFUNGUKIA UWAZI
Akizungumza na Uwazi msibani hapo, Faudhia alisema:
“Siku ya tukio ambayo ilikuwa Juni 18, Munila alikojoa kitandani ndipo wifi alimtoa sebuleni na kuanza kumchapa kwa kutumia mkanda. Alipoona mtoto ametulia, aliniita na kuniambia Munili alianguka hivyo niende nikamwite nesi anayemiliki duka la dawa mtaani, nilimwona Munili akitokwa povu mdomoni, jeraha la kupigwa na mkanda kwenye paji la uso na shingoni, nilipomuuliza alipatwa na nini akaniambia alianguka.
“Nilipofika kwa nesi akaniambia kama mtoto alizidiwa tumpeleke hospitali, nilirudi nyumbani na kumweleza wifi, ndipo akachukua maji ya baridi na kummwagia Munili lakini hakuamka, alichukua kitenge akampepea lakini Munili alitulia kimya.
Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Mpakani wakiwa wameubeba mwili wa marehemu Munili.
“Wifi akanituma niende kumwita mama Aneth  ambaye ni jirani, alipofika alimwangalia mtoto akashauri akaitwe mjumbe ambaye hakuwepo. Nikamfuata Shehe Mpitanga ambaye alipofika na kumwangalia mtoto akasema alishafariki dunia, wifi akaanza kulia.”
Faudhia aliongeza kuwa, alipowaeleza ukweli akina mama kuhusiana na tukio hilo, wifi yake alitoka ndani na kutaka kutoroka lakini walifanikiwa kumnasa ndipo nilichukuliwa mimi, kaka (baba wa marehemu), tukapelekwa tena polisi ambako nilieleza kilichotokea, wakaamua kuwashikilia wao hadi leo (Juni 21, mwaka huu).
KAMANDA WA POLISI AZUNGUMZA
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura alipopigiwa simu na kuulizwa kama alikuwa na taarifa ya mauaji hayo alisema hakuwa na taarifa ila atafuatilia.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!