Saturday, 28 June 2014

KASI YA MAJAMBAZI IDHIBITIWE!

KATIKA siku za hivi karibuni, matukio ya ujambazi yanayoambatana na mauaji na uporaji wa mali, yanaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.


Hali hiyo imetulazimu kwa mara nyingine kuandika tahariri hii, kuliomba Jeshi la Polisi liongeze nguvu, maarifa na weledi katika kukabiliana na kasi hiyo ya ujambazi.
Matukio ya hivi karibuni, likiwemo la kuuawa kwa sista wa Kanisa Katoliki na mfanyabiashara kule Geita mchana kweupe na kupora fedha pamoja na mengine, ndiyo yaliyotupa msukumo wa kuzungumzia janga hili leo.
Hakuna ubishi kwamba usalama wa watu na mali zao sasa uko shakani na hata kile ambacho kimekuwa kikihubiriwa na serikali usiku na mchana, kwamba taifa lina amani na utulivu, kiuhalisia hakiko hivyo.
Sisi tunathubutu kusema pasipo shaka kwamba taifa linakabiliwa na janga la ujambazi, umwagaji wa damu, udokozi na ukatili usiovumilika, na lazima tukuchuke hatua sasa.
Msingi wa kauli hii ni kuibuka kwa kasi kwa vitendo vya uporaji wa fedha vinavyofanywa na majambazi wenye silaha za moto huku kukiwa hakuna taarifa za kuridhisha za kukabiliana na matukio hayo kutoka taasisi za ulinzi na usalama.
Tunajiuliza kwanini matukio haya ya kinyama yameibuka kwa kasi kubwa kipindi hiki wakati miezi nichache nyuma hali haikuwa ya kutisha kwa kiwango hiki?
Tafakuri yetu katika swali hili inatulazimisha kuwageukia wana usalama wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao na kuwaasa watende kazi zao za kiulinzi kwa mbinu za kisasa zaidi ili waweze kukomesha ukatili huu unaohatarisha amani na utulivu wa taifa letu kwa sababu tunaamini majambazi nao sasa wanatekeleza uhalifu wao kwa mbinu za kisasa zaidi.
Haitoshi kwa wana usalama kutangaza katazo kwa waendesha pikipiki, maarufu zaidi kwa jina la bodaboda, kutoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kubainika kuwa aina hiyo ya usafiri ndiyo inayotumiwa zaidi nyakati hizi na majambazi kutekeleza vitendo vyao vya kinyama, bali hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa, lengo likiwa kuepusha umwagikaji wa damu ya Watanzania.
Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kubadili mbinu linazozitumia sasa kupambana na majambazi ambazo zina dalili za kushindwa na badala yake lijikite kwenye utendaji wa kileo unaojengwa katika misingi ya matumizi ya teknolojia inayorahisisha utekelezaji wa kazi na inayotoa majibu ya uhakika kwenye matukio magumu na tata kama haya yanayoendelea kutokea sasa hapa nchini.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!