MANISPAA ya Ilala imeanza kuadhimisha Siku ya Mazingira kwa kupanda miti 100 kati ya 1,252 inayotarajiwa kupandwa ifikapo Juni 5, siku ya kilele cha maadhimisho hayo.
Akizungimza wakati wa shughuli hiyo iliyofanyika Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Ilala, Elizabeth Thomas, alisema miti hiyo aina ya mitende mbali na kupendezesha mji inaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Alisema ina uwezo mkubwa wa kunyonya hewa ya ukaa inayozalishwa zaidi na magari, viwanda, mitambo na mashine mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alisema tatizo la mazingira ni mgogoro wa kidunia ambapo hata wanasayansi hawajaja na tiba muafaka.
Alisema madhara ya mvua yaliyojitokeza siku za karibuni yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo kupanuka kwa kingo za mito kunakosababishwa na uchimbaji wa mchanga.
Kwamba kila shughuli aifanyayo binadamu inachangia uharibifu wa mazingira, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuyatumia mazingira hayo katika njia iliyo endelevu.
Mwakilishi wa Mfuko wa Burhan Tanzania, Zanuddin Adamjee, ambao wamegharamia kununua miti hiyo kwa sh milioni 30, ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika suala zima la utunzaji mazingira
No comments:
Post a Comment