Saturday, 14 June 2014

BAJETI YACHANWA CHANWA!

SIKU moja baada ya kusomwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali, wanasiasa na wataalamu mbalimbali wametoa maoni yao kwa kuikosoa bajeti hiyo, wakisema haina jipya na imefanywa bila kufanyiwa utafiti wa kina kwa lengo la kukidhi hali halisi ya Watanzania.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kwa ujumla bajeti hiyo haina jipya kwa kuwa hakuna vyanzo vingine vya mapato na walivyoainisha  ni vile vilivyozoeleka, huku akitolea mfano kupandishwa kwa sigara, vinywaji baridi na vinywaji vikali.
Hata hivyo, alisema walichoingiza kipya ni kuhusu kutoingiza magari ya mitumba, jambo ambalo aliliita kuwa ni ubabaishaji kwa kuwa si Watanzania wote wanaoweza kununua magari mapya.
“Hii si kweli, huwezi kwa maisha ya Mtanzania ukamwambia kuwa usinunue gari la mitumba, nani atakayeweza kumudu kununua gari kwa dola 6,000 au ndiyo kufanya jitihada za kupunguza magari katika Mkoa wa Dar es Salaam?” alihoji Dk. Bana.
Alisema bajeti hiyo imeangalia zaidi wananchi wa mjini na kuwasahau wa vijijini, hasa katika masuala ya manunuzi ya saruji, mabati kwa kuwa kule wananunua kwa bei kubwa ukilinganisha na mijini.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa, alisema bajeti inatakiwa kujibu mapigo ya masikini na ndiyo anayoikubali, lakini pia kuna changamoto kubwa katika upatikanaji wa fedha hizo zilizoainishwa.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, alisema bajeti ni ile ile ya enzi na enzi ya kutegemea vinywaji sigara na bia, haina jipya.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati, alisema bajeti hiyo inatisha kwa kuwa ni tegemezi, wafadhili wanaweza kutoa au kutokutoa fedha.
TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!