Friday, 13 June 2014

BAJETI 2014/2015 KODI YA MISHAHARA YAPUNGUA KIDUCHU, MISHAHARA JUU

Kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi nchini kutaka Kodi ya Mshahara (Paye), ipunguzwe hadi chini ya asilimia 10 kimekwama baada ya Serikali kupunguza kodi hiyo kwa asilimia moja.
Hata hivyo, Serikali katika bajeti yake ya 2014/15 iliyosomwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya imetangaza ongezeko la kima cha chini cha mishahara ambacho kiwango chake hakikubainishwa.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum alisema katika mwaka huo unaoanza Julai Mosi, mwaka huu Serikali inakusudia kufanya marekebisho katika mfumo wa ‘Paye’ kwa kupunguza kiwango cha kodi kutoka asilimia 13 hadi 12.
Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa na Bunge, wafanyakazi watapata unafuu kiduchu wa kodi ambao ni sawa na Sh1, 900.
Kodi hiyo ya mishahara imekuwa kitanzi kwa wafanyakazi na Rais Jakaya Kikwete alipohutubia taifa katika sherehe za Mei Mosi, Mwaka huu aliahidi kuendelea kushughulikia kilio hicho kadri mapato ya Serikali yanavyoruhusu.
“Kumekuwepo pia na ombi la muda mrefu la kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kuwa chini ya asilimia 10. Kama nilivyoahidi mwaka jana, hili tutaendelea kulishughulikia kadri uwezo wa Serikali utakaporuhusu.
“Tumeshafanya hivyo kabla na hatuna sababu ya kutofanya hivyo huko tuendako. Tayari tumepunguza kutoka asilimia 18.5 mwaka 2007 hadi asilimia 13 hivi sasa. Maombi yenu tumeyapokea, tuachieni, tuangalie nini tunachoweza kufanya kama miaka iliyopita.”
Rais Kikwete alisema kinachokwamisha punguzo hilo kufikia tarakimu moja ni uwezo mdogo wa mapato ya Serikali.
Kima cha chini
Katika hotuba hiyo ya bajeti, Waziri Mkuya alitangaza mpango wa Serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma lakini hakutaja ongezeko hilo litakuwa la kiwango gani.
Suala la ongezeko la mishahara pia lilielezwa na Rais Kikwete wakati wa Mei Mosi, alipobainisha uwezekano wa nyongeza ya mwaka huu kuwa kubwa kuliko ya mwaka jana.
“Najua kuwa nyongeza tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi nisingependa iwe hivyo.”
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!