Wakati wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu duniani kote wameshaanza kuufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, Bacary Sagna beki wa timu ya taifa ya Ufaransa ameeleza kinagaubaga kwamba, ataendelea kufunga saumu ya mwezi huo, licha ya kukabiliwa na kibarua kigumu cha mashindano ya kombe la dunia ambayo yameingia hatua ya pili ya mtoano. Sagna amesisistiza kwamba, ataendelea kufunga saumu ya mwezi mtukufu, licha ya kukabiliwa na mechi ngumu kwenye michuano hiyo. Sagna ameviambia vyombo vya habari vya Ufaransa na hapa tunamnukuu: 'Mimi nataka kufunga saumu nchini Brazil, kwa kuwa ni Muislamu. Dini tukufu ya Kiislamu inanipa fursa ya kutofunga saumu nikiwa katika mazingira maalumu kama vile safari na maradhi, lakini pamoja na kukabiliwa na mashindano ya kombe la dunia nchini Brazil sitaki kufungulia. Nitaendelea kufunga saumu ya mwezi mzima wa Ramadhani, Inshaallah', mwisho wa kunukuu. Licha ya Bacary Sagna wachezaji wengine wengi wanaoozichezea timu za taifa za Ufaransa,
Algeria, Nigeria na Ujerumani wameendelea kusisitiza kwamba watafunga saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani licha ya kukabiliwa na mechi ngumu za kombe la dunia. Hapo kesho, Nigeria 'Tai wa Kijani' itapimana misuli na Ufaransa, huku timu ya taifa ya Algeria 'Mbweha wa Jangwani' itajitupa uwanjani siku ya Jumanne kupambana na Ujerumani katika hatua ya 16 bora. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni Jiri Dvorak mjumbe mwandamizi wa Kamati ya Afya ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA alisema kuwa, wachezaji Waislamu watakaofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, hawataathirika kiafya wakati wa kuendelea michuano hiyo nchini Brazil.
1 comment:
aziz bilal14:36
1
Reply
Muislam ni muislam tuu,wanasema ukizaliwa muislam hakuna kitu au sababu zozote zile zitakazokuzuia kufanya ibada zako,mimi binafsi ninamuombea mwenyezi mungu azidi kumjalia na ikiwezekana afanikishe maombi yake yote,inshaallah khayri
Post a Comment