Thursday 5 June 2014

ASILIMIA 33 YA WATOTO WANAUPUNGUFU WA VITAMIN A

TAASISI ya Chakula na Lishe Tanzania, imesema asilimia 33 ya watoto walio na umri chini ya miaka 5 nchini wana upungufu wa vitamini A.

Mtaalamu wa chakula na lishe kwa watoto wachanga na wadogo, Neema Joshua, alibainisha hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari, hivyo kuwahimiza wazazi na walezi wenye watoto wadogo kutambua umuhimu wa vitamini A katika ukuaji na maendeleo mazuri ya afya na uhai wa mtoto.
“Hali hii inatokana na kuwapa watoto vyakula visivyokidhi mahitaji ya vitamini A, kwani hula kiasi kidogo wakati mahitaji yao ni makubwa, na hivyo ni muhimu wapatiwe ulaji wa vyakula vyenye virutubisho, hasa vya vitamini A kwa wingi,” alisema Neema.
Pia alisema asilimia 37 ya kinamama walio katika umri wa kuzaa wana upungufu wa vitamini A.
Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Elifatio Towo, alisema madhara ya upungufu wa vitamin A mwilini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi, ni kutokuona vizuri kwenye mwanga hafifu, upofu na maradhi ya mara kwa mara.
“Vitamini A ni mojawapo ya vitamini isiyotengenezwa na mwili, hivyo ni lazima itokane na vyakula ambavyo ni mboga na matunda, hasa yenye rangi ya kijani na njano, samaki hasa dagaa, mafuta ya mawese, maini na viazi lishe,” alisema Elifatio.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!