Saturday, 7 June 2014

ALIYETELEKEZWA KWA SARATANI AFARIKI

 Mgonjwa wa saratani ambaye alidai kupewa tiba feki za mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (OCRI), Pendo Shoo amefariki dunia  juzi wilayani Karatu akiwa safarini kuelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro kwa wazazi wake.
Mdogo wa Pendo, Digna Shoo, alisema dada yake alifariki juzi, saa nne usiku wakati wanafamilia wakimfanya maombi.
“Alianza kubadilika ghafla wakati tukiwa katikati ya maombi, alilegea na mgongo wake ukawa kama unapinda hivi, tukamshika na tukamweka kitandani,” alisema.
 Digna alisema kwamba baada ya kumweka kitandani  mtumishi wa Mungu aliyekuwa nyumbani hapo alimwombea na hazikupita dakika nyingi akakata roho. Alisema Pendo alikwenda Karatu akitokea Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita, kipindi ambacho hali yake ilikuwa imeshatetereka sana kiasi cha kushindwa kutembea mpaka apate msaada wa mtu karibu.
“Wakati tunatoka Dar es Salaam kuja Karatu, hali yake ilikuwa imeshakuwa mbaya, alikuwa hawezi kutembea bila kumpa ‘support’ (msaada) alikuwa anapepesuka,” alisema Digna.
Digna alisema safari ya dada yake haikuwa imelenga kuishia Karatu, bali walikuwa wanaelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro ambako ni nyumbani kwao alipozaliwa, lakini mauti yalimkuta msichana huyo kabla hajafika.
Kwa maelezo ya Digna, Pendo alikuwa amekata tamaa ya kuishi kutokana na saratani hiyo kusambaa katika matiti yake mawili na kumsababishia vidonda vilivyompa maumivu makali.
Itakumbukwa kwamba gazeti hili liliwahi kuripoti mara mbili taarifa kuhusu Pendo; kwanza ni ile iliyohusu mgonjwa huyo kupewa dawa feki ambazo badala ya kumtibu zilimsababishia madhara zaidi na pili ni kuhusu kunyanyapaliwa baada ya taarifa ya awali kuandikwa gazetini.
Pendo alianza kupata tiba OCRI Novemba mwaka jana baada ya kupata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini katika mchakato wa tiba yake,  alitozwa kiasi cha Sh1.34 milioni na mtumishi wa OCRI, Almasi Matola kinyume na taratibu.
Baada ya gazeti hili kuchapisha habari hiyo, Mei 20 mwaka huu alikwenda katika hospitali hiyo kupata tiba zaidi, lakini alinyanyapaliwa na wahudumu wa OCRI na akielezwa kwamba vipimo alivyochukuliwa awali vilikuwa havionekani.
 “Niliamua kurudi hospitali nikapime tena na nilitoa damu kwa ajili ya vipimo, lakini nilipokwenda tena kuchukua majibu walidai damu yangu imepotea. Kwa hiyo nililazimika kuanza upya, nilitoa damu tena na vipimo vyote vikawa tayari kama X-ray, Ultra sound na nikavipeleka kwa daktari,” alisema Pendo kabla ya kukutwa na mauti.
Alisema alipatwa na hofu zaidi baada ya kwenda kwa daktari wake Dk Dominista Kombe, ambaye alipaswa kumpa matokeo ya vipimo, lakini alishangaa daktari huyo alipomjibu kwamba, “Majibu yako utayajua hukohuko,” akimaanisha kwenye chumba cha tiba ya mionzi.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!