Thursday, 1 May 2014

WAFUNGWA WANAOTOKA KWA MSAMAHA WA RAIS HURUDI TENA GEREZANI"

 
Ripoti mpya ya utafiti imebainisha kuwa jitihada za Rais Jakaya Kikwete kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani kwa kutoa msamaha zinahitaji kufanyiwa marekebisho kwani zaidi ya asilimia 30 ya wanaonufaika nayo hurudi tena magerezani kwa makosa tofauti.
Ripoti hiyo iliyotolewa Dar es Salaam jana na Shirika lisilo la Serikali linaloshughulikia masuala ya wafungwa Tanzania (IRaWS-T), imesema tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005 hadi sasa, ameshasamehe wafungwa 62,336 lakini bado kuna idadi kubwa hurudi magerezani baada ya kukamatwa na makosa mbalimbali.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk James Jesse alisema utafiti huo ulikusanya taarifa kutoka mikoa ya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam kati ya Agosti 2013 na Machi 2014.
“Msamaha wa Rais umepunguza sana wafungwa magerezani, lakini uchaguzi wa wafungwa wanaotakiwa kuachiwa huru hauangalii athari zao kwa jamii, hivyo wanarudi tena magerezani,” alisema Dk Jesse.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 45 kifungu cha 1(b) inampa Rais mamlaka ya kusamehe wafungwa ambao wametimiza vigezo mbalimbali vilivyowekwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafungwa wanaoachiwa huru wafikapo mitaani hukosa uangalizi wa karibu na msaada wa kuwawezesha kuishi katika maadili yanayofaa, badala yake polisi huwaona kuwa wahalifu na kuwatuhumu kwa kila kosa linalotokea.
“Bahati mbaya neema hii inayotolewa na Rais ni njia tu inayotumika kupunguza wafungwa. Njia nyingine zilizoanzishwa tangu mwaka 1987 hazitazamwi ikiwamo ile ya wafungwa kufanya kazi katika jamii,” alisema.
Ripoti inaeleza kuwa wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961 kulikuwa na magereza 72 yaliyokuwa yakichukua wafungwa 11,965, lakini tangu wakati huo idadi ya wafungwa imekuwa ikiongezeka huku ujenzi wa magereza ukishindwa kwenda sambamba na ongezeko hilo.
Mwaka 2002 umetajwa kuwa ndiyo uliokuwa na kiwango kikubwa zaidi cha wafungwa magerezani kwa kuwa na wafungwa 45,000 kwenye vyumba vilivyotakiwa kuwa na watu 22,669 pekee. Hata hivyo, idadi hiyo imeshuka hadi kufikia 29,552 Aprili mwaka huu.
Pia, utafiti huo umebaini ongezeko kubwa la wafungwa kwenye magereza makubwa nchini na asilimia zake kama yanavyoonekana kwenye mabano Ukonga (63), Keko (36.7), Isanga-Dodoma (74.4) na Butimba Mwanza (41.9).
Ripoti hiyo ya IRaWS-T, Taasisi inayoundwa na maofisa magereza wastaafu, imependekeza Serikali kuangalia mifumo ya kushughulikia wafungwa inavyofanywa na nchi nyingine ambazo zimepunguza misongamano magerezani kwa kiasi kikubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa IRaWS-T, John Nyoka alisema Tanzania inatakiwa itumie mfumo wa kupunguza msongamano wa wafungwa (ODS), unaotumiwa na Kenya, Zambia, Nigeria, Afrika Kusini na Zambia, ambao huzingatia athari ya mfungwa kwa jamii na si urefu wa kifungo...

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!