KIU ya Malawi ya kupata Rais wa nchi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Mei 20, mwaka huu, huenda ikashindwa kukatika miongoni mwa raia wa nchi hiyo baada ya Rais anayemaliza muda wake, Dk Joyce Banda kutangaza kusitisha shughuli zote za uchaguzi huo.
Banda aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka miwili kuanzia Aprili 7, mwaka 2012, alikuwa miongoni mwa wagombea wanne wa nafasi ya urais. Banda maarufu kama JB, aliingia kwenye uchaguzi kwa tiketi ya chama chake cha People’s (PP).
Mgombea mwingine ni Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Peter Mutharika wa chama cha Democratic (DPP).
Mbali ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1970, Mutharika (65) amefundisha pia katika vyuo vikuu vya Haile Selassie (Ethiopia), Rutgers (Marekani), Makerere (Uganda) na Washington (Marekani).
Pia ni Mhadhiri anayefundisha kwa muda katika Shule ya Uchumi ya London, Uingereza. Wagombea wengine ni Mchungaji Dk Lazarus Chakwera (59) wa chama kikongwe cha Malawi Congress (MCP) na Atupele Muluzi wa chama cha United Democratic Front (UDF).
Hata hivyo, baada ya siku mbili za kusubiri matokeo, huku taarifa zikisambaa kwa kasi kwamba Rais huyo anaelekea kushindwa uchaguzi, jana aliibuka na kuamuru kusitishwa mara moja kwa shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo mkuu wa nchi hiyo.
Akizungumza katika Ikulu yake jijini Lilongwe jana, Banda mwenye umri wa miaka 64, ameamuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi (MEC ) kusitisha shughuli hiyo na kutangaza kuwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, utarudiwa ndani ya siku 90 kuanzia jana.
“Baada ya kujiridhisha kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, kwa maslahi ya wananchi wa Malawi, shughuli zote za uchaguzi zinasitishwa. “
Mimi, Dk Joyce Banda, Rais wa Malawi kwa mamlaka ya kikatiba niliyopewa kupitia Kifungu 88 (2) cha Katiba, natangaza kusitisha taratibu zote za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ikiwa pamoja na kuhesabu kura na kutangaza matokeo yake.
“Hivyo, natangaza uchaguzi mpya wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika ndani ya siku 90 kuanzia leo (jana Mei 24),” imeeleza sehemu ya taarifa ya Rais Banda kwa vyombo vya umma jana.
Aidha, alikwenda mbali zaidi na kusema yeye binafsi, hatakuwa miongoni mwa wagombea urais katika uchaguzi huo wa marudio. Katika maelezo yake, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo, kwa kile alichokiita ni kuvurugika kwa mtiririko mzima wa shughuli za upigaji kura, kuhesabu na hata namna ya kusimamia utoaji wa matokeo yake. Kwa ujumla, ameuita ulikuwa uchaguzi uliojaa `mchezo mchafu’.
Kutokana na amri ya Rais huyo wa nne wa Malawi, Mwenyekiti wa MEC, Jaji Mackson Mbendera alisema anawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuona kama utekelezaji wa amri hiyo ya Rais Banda, hautavunja Sheria ya Nchi.
Awali kabla ya amri hiyo, MEC ilianza kutangaza matokeo ambayo yalionesha Profesa Mutharika, mwanazuoni aliyebobea katika masuala ya sheria, alikuwa akiongoza.
Mutharika pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, aliyeshika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali, zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.
Katika matokeo ya awali ya MEC, yaliyobeba asilimia 30 ya kura zote zilizohesabiwa na kupokelewa katika ofisi kuu za tume hiyo, yalionesha Mutharika, mdogo wa aliyekuwa Rais wa tatu wa Malawi, Bingu wa Mutharika, alikuwa anaongoza kwa kupata 683,621 akifuatiwa na Banda kura 372,101.
Mgombea wa MCP, Mchungaji Chakwera alikuwa na kura 289,145 huku Muluzi akiwa na kura 269,250.
Muluzi ni mtoto wa Rais wa Pili wa Malawi, Bakili Muluzi na ndiye mgombea kijana zaidi akiwa na umri wa miaka 35.
Kabla ya kujitosa kwenye urais, alikuwa Waziri wa Uchumi, Mipango na Maendeleo katika Serikali ya Rais Banda.
Akizungumza na wanahabari juzi usiku, Jaji Mbendera alisema Tume yake kwa pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa, wamethibitisha matokeo hayo.
Jaji Mbendera alisema Tume yake, imegundua kuwa kulikuwa na udanganyifu katika baadhi ya maeneo, ambapo wamekuta idadi ya kura zilizopigwa ni zaidi ya watu walioandikishwa kupiga kura.
Alisema wamezuia matokeo hayo hadi watakapopata ufumbuzi na ukweli wa taarifa hiyo. Wakati matokeo hayo yanaanza kutangazwa, Mahakama nchini humo imezuia uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) kumlazimisha Mkurugenzi Mkuu, Dk Benson Tembo kwenda likizo ya lazima na haraka. Uamuzi huo umetokana na baadhi ya wanasheria kutoka Tume ya wanasheria wa Malawi, kuweka zuio mahakamani kupinga uamuzi wa bodi ya shirika hilo.
Juzi asubuhi, Dk Tembo alipewa barua ya kumtaka aende likizo ya lazima, akidaiwa kushindwa kufuata maelekezo ya serikali, ambayo ni pamoja na vyombo vya shirika hilo ikiwemo televisheni na redio za taifa, kuendelea kutoa matokeo ya uchaguzi, ambayo hayajathibitishwa na MEC.
Inadaiwa MBC pia ilishindwa kurusha moja kwa moja matangazo ya mkutano wa Rais Banda na wanahabari mjini Lilongwe, uliofanyika Alhamisi iliyopita, ambapo Dk Banda alikuwa akitoa maelekezo kwa MEC kuanza kuhesabu kura kwa kutumia mikono na kuzuia kutoa matokeo, kutokana na udanganyifu uliojitokeza.
Rais alisema kuwa uchaguzi huo umekumbwa na visa vingi, ikiwemo wizi wa kura na udukuzi kupitia mitambo ya kujumlisha kura Wakati hayo yakitokea, Mutharika anayeonekana kujiamini, aliwataka wafuasi wake na wananchi wa Malawi, kuwa watulivu wakati taratibu nyingine zikisubiriwa kufuatwa.
CRD: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment