Hatimaye Tume ya uchaguzi nchini Malawi imeanza kutoa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo jumanne iliyopita.
Matokeo hayo ambayo ni asilimia 30 tu ya kura ambazo zimehesabiwa hadi sasa yanaonyesha kuwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani Democratic Progressive Party-DPP Profesa Peter Mutharika anaongoza kwa kura 683,621 akifuatiwa na Dr Joyce Banda wa Peoples Party kwa kura 372,101
Mgombea Urais wa chama kikongwe cha kisiasa nchini humo, Malawi Congress Party MCP Mchungaji Dr Lazarus Chakwera anashika nafasi ya tatu kwa kujipatia kura 289,145 huku Atupele Muluzi wa United Democratic Front- UDF akikusanya kura za wamalawi 269,250
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza ambaye anafuatilia uchaguzi huo nchini humo, amesema mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mackson Mbendera aliwaambia waandishi wa habari mjini Blantyre usiku wa kuamkia leo kuwa tume yake kwa pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa wamethibitisha matokeo hayo.
Udanganyifu
Katika mkutano huo Jaji Mbendera amesema tume yake imegundua kuwa kulikuwa na udanganyifu katika baadhi ya maeneo ambapo wamekuta idadi ya kura zilizopigwa ni zaidi ya watu walioandikishwa kupiga kura, na kwamba wamezuia matokeo hayo hadi watakapo pata ufumbuzi na ukweli wa hali ilivyokuwa.
Wakati huo huo Mahakama nchini humo imezuia uamuzi wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la utangazaji la Malawi MBC kumlazimisha Mkurugenzi Mkuu Dr Benson Tembo kwenda likizo ya lazima na haraka.
Uamuzi huo umefuatia baadhi ya wanasheria kutoka kamisheni ya wanasheria wa Lilongwe kuweka zuwio mahakamani kupinga uamuzi wa bodi ya shirika hilo.
Itakumbukwa kuwa ijumaa asubuhi Dr Tembo alipewa barua ya kumtaka aende likizo ya lazima kutokana na madai kuwa ameshindwa kufuata maelekezo ya mwajiri wake ambaye ni serikali.
Miongoni mwa madai hayo ni pamoja na vyombo vya shirika hilo ikiwemo television na radio za taifa kuendelea kutoa matokeo ya uchaguzi ambayo hayajathibitishwa na Tume ya uchaguzi.
Pia MBC ilishindwa kurusha moja kwa moja matangazo ya mkutano wa Rais Joyce Banda na waandishi wa habari mjini Lilongwe siku ya alhamis, ambapo Dr Banda alikuwa akitoa maelekezo kwa tume ya uchaguzi kuanza kuhesabu kura kwa kutumia mikono na kuzuia kutoa matokeo kutokana na udanganyifu uliojitokeza
CHANZO: MATUKIO NA VIJANA BLOG
No comments:
Post a Comment