Saturday, 3 May 2014

MAFUTA YA KULA YALIYO JUANI SUMU


     

WANANCHI wametakiwa kuacha kununua mafuta ya kula, yanayouzwa yakiwa yamewekwa juani, kutokana na kuwa na athari kubwa kiafya, ikiwemo kusababisha ugonjwa wa saratani.


 Mkaguzi wa Chakula kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati, Albert Deule alisema hayo juzi wakati akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Kibaigwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Alisema ni vyema wauzaji wa mafuta hayo, wakaweka mafuta hayo mbali na jua, kwani kitendo cha kuuza mafuta yakiwa yameanikwa juani, kina athari za kiafya kwa watumiaji.
Deule alisema jua husababisha mafuta kuchacha na hutengeneza sumu, inayoweza kuleta madhara mwilini, ikiwemo kusababisha saratani.
Alisema mafuta ambayo tayari yamechacha na kisha kwenda kuchemshwa, madhara yake ni makubwa mwilini.
“Wananchi msinunue bidhaa zilizoanikwa juani, ni hatari kiafya, njia sahihi ni mteja kusema hapana, watu wengi wanapata magonjwa ya tumbo kwa kutumia mafuta yasiyofaa, ni muhimu bidhaa zikawekwa mahali salama wakati zinauzwa,” alisema.
Pia, alisema ni muhimu kwa wajasiriamali, kutafuta namna nzuri ya kufungasha mafuta na sio kama sasa, ambapo hata chupa za maji zilizotumika zimekuwa zikitumika kuuzia mafuta.
Alisema chupa nyingine, huwa si salama, kutokana na kutumika kwa matumizi mengine na ndipo hutumika tena kwa ajili ya kuuzia mafuta.
“Vifungashio ni tatizo kwa wajasiriamali, lakini ni lazima wajali afya za walaji na wateja wahakikishe wanakagua bidhaa muda ulipotengenezwa na muda wa mwisho wa matumizi ya bidhaa hizo,” alisema.
Mkaguzi huyo wa chakula alisema ni muhimu wafanyabiashara, wakafuata utaratibu kabla ya kuanza biashara ili kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa, tofauti na sasa ambapo wengi wanaanzisha biashara ya usindikaji wakiwa hawana mahali maalumu pa kufanyia biashara zao huku mazingira ya biashara, yakiwa hayaridhishi.
Alisema wajasiriamali wa usindikaji ni lazima wazingatie usafi na kama biashara ya kukoboa na kusaga nafaka inaendeshwa bila kuwa na choo, hakuna mbadala, biashara hiyo wataifunga tu.
“Mfanyabiashara asiye na choo, hana msamaha, peleka sokoni bidhaa inayofaa,” alisema. Alisema kisheria shughuli za usindikaji, zinatakiwa kuwa na mtaalamu anayesimamia shughuli zote ili bidhaa zinazozalishwa ziwe bora.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!