Kwa miaka mingi sana binadamu wa karne zote wamekuwa wakitafuta siri za maisha marefu, kuzuia uzee na hata kuzuia kifo.
Lakini pamoja na jitihada nyingi mambo haya yameendelea kuwa changamoto kubwa kwenye maisha ya mwanadamu katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa Tanzania, inakadiriwa kuwa umri wa kuishi kwa wanaume ni takriban miaka 58.2 na kwa wanawake ni miaka 60.5.
Muda huu wa kuishi ni mfupi sana ikilinganishwa na wenzetu katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani ambako wastani wa kuishi ni unakadiriwa kuwa ni miaka 78.2.
Wanasayansi wamekuwa na nadharia nyingi kuhusu sababu zinazosababisha binadamu azeeke na kufa mapema. Ila wengi hufikiri kuwa tunazeeka mapema kutokana na sababu za maumbile na vinasaba tunavyorithi kwa wazazi wetu.
Wengine husema kuwa tunazeeka haraka kutokana na kuwa na mtindo usiofaa wa maisha.
Mtaalamu wa Afya, Dk Mark Stibich anasema kwamba kuzeeka haraka na kuishi maishi mafupi ni suala mtambuka na linahusisha mambo kama vile vinasaba, kemia, fiziolojia ya mwili pamoja na tabia zetu kwa mujibu wa makala yake ya Mei 10, 2014 liyowekwa kwenye tovuti yalongevity.about.com.
Mtaalamu wa maabara nchini Ujerumani, Dk James Vaupel anadai kuwa vinasaba huchangia kasi ya kuzeeka kwa asilimia tatu pekee na sehemu kubwa ya visababishi vya kuzeeka haraka hutokana na mtindo wa maisha usiofaa pamoja na lishe duni.
Dk Vaupel anaongeza kusema kuwa tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hata pacha wanaozaliwa siku moja, hupishana urefu wa maisha kwa karibu miaka 10 kutokana na kuwa na mitindo tofauti ya maisha.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wakazi wa maeneo wanaoishi maisha marefu zaidi duniani kama vile Japani, Italia na Marekani, pamoja na mambo mengine, wanajiepusha na matumizi ya vileo, tumbaku na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu.
Pia huvuta hewa safi ya kutosha na kupata mapumziko ya kutosha baada ya kazi ngumu kila siku.
Watu hawa pia huwa na mtazamo chanya wa maisha, mazoezi na chakula asilia cha mimea kama vile mbogamboga na matunda kwa wingi
No comments:
Post a Comment