WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewazawadia washindi wa Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani Sh 500,000 kila mchezaji, huku akiwaongezea kidogo wachezaji watatu waliong’ara nusu fainali na fainali.
Timu hiyo ya watoto wenye umri chini ya miaka 16, ilipangwa Kundi la 2 pamoja na Argentina, Nicaragua, Philippines na Burundi na kulikuwa na makundi matatu.
Tanzania iliingia nusu fainali kwa kuwa mshindi wa pili na pia kumenyana na Marekani na kuichapa mabao 6-1 na baadaye kuitoa Burundi kwa mabao 3-1.
Pinda alitangaza zawadi hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma jana, alipokutana na washindi hao kwa chakula cha mchana na kuwapongeza kwa kuitangaza Tanzania vyema.
“Mmetupa heshima kubwa sana na nimeona tusiishie kwa kuwaona bali mpitie katika Bunge Maalumu wajumbe watafurahi kuwaona. Changamoto mliyotupa ni kubwa sana kwangu binafsi, kwa viongozi na Wizara,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Wachezaji walioongezewa kidogo zaidi ya Sh 500,000 ni Kipa Bora, Emmanuel Chaka, aliyepewa kombe na mfungaji wa mabao manne katika nusu fainali dhidi ya Marekani, Michael Simon.
Mwingine aliyeongezewa zawadi ni mfungaji wa mabao yote matatu ya fainali dhidi ya Burundi, Frank Willium. Kabla ya kuanza kuzungumza, Pinda alitoa nafasi kwa mmoja wa watoto hao, Majuto Ismail, aeleze hali ilivyokuwa katika michuano hiyo mpaka wakafikia mafanikio hayo.
Majuto aliyecheza katika michuano iliyopita Afrika Kusini na kuwa washindi wa pili na katika michuano hii, alikwenda kama Meneja, alisema walipofika Brazil katika Jiji la Rio de Janeiro, walikuwa timu ya sita kufika.
Mashindano yalipoanza alisema walicheza kwa kujituma na walikuwa na nidhamu nzuri kwa kufuata sheria, kiasi ambacho kama kungekuwa na zawadi ya nidhamu wangepewa.
Baada ya kushinda, Majuto alisema walikwenda kutembelea vivutio vya Brazil, ikiwemo wanakoishi watoto wa mazingira hatarishi.
Majuto aliyesema kuwa hapendi kuitwa mtoto wa mitaani kwa kuwa mtaa hauzai, alitakiwa na Pinda kufafanua hilo eneo walilokwenda linafanana na eneo gani Tanzania, na akajibu linafanana na Mwanza ambako yeye amekulia katika mazingira magumu.
Akifafanua kuhusu dhana ya maisha ya watoto wa mazingira magumu katika nchi zilizoendelea na nchi masikini, Pinda alisema hata jina Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani halipendi, lakini ndivyo linavyoitwa.
Alifafanua kuwa watoto hao ni ambao hawajakua katika mazingira nadhifu na kupata mapenzi ya baba na mama. Alisema pamoja na mazingira hayo, watoto hao wametoa funzo kuwa hata katika mazingira magumu, wameonesha karama zao na kuleta heshima kwa Taifa na kazi iliyopo ni kukuza karama zao.
“Msikate tamaa kwa kuitwa hivyo, inaonekana kama vile tusi, lakini ni aina ya uhalisia ambao mmeutumia kuleta kitu kizuri,” alisema Pinda na kuongeza kuwa atawasiliana na uongozi wa Mkoa wa Mwanza wawape mapokezi mazuri na yeye akitembelea mkoa huo, atakwenda kuwaona.
Katika hatua nyingine kabla ya kuonana na Pinda, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliamua kuchangia timu hiyo ya watoto wa mitaani.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan, alisema jana wataandaa utaratibu kwa wajumbe wa Bunge hilo wanaopenda kuwachangia watoto hao kufanya hivyo.
Alisema hayo alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo, aliyeomba wajumbe wa Bunge Maalumu, wawachangie watoto hao waliopeperusha vyema Bendera ya Tanzania nchini Brazil.
Watoto hao walifika jana katika Bunge Maalumu na kutambulishwa kuwa wageni wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alifananisha washindi hao na timu ya Mathare United ya Kenya ambayo iliundwa na watoto wa mitaani na baadaye kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki.
Alisema timu hiyo ilitunzwa na kutoa wachezaji wazuri akiwemo Victor Wanyama ambaye leo anacheza katika ligi kubwa duniani, Ligi Kuu ya England katika klabu ya Southampton.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete ameipongeza timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kwa kutwaa Kombe la Dunia jijini Rio de Janeiro, Brazil.
“Mmetuwakilisha vyema, ninawapongeza sana, pia mmewapa moyo watoto wengine wote wenye vipaji maalumu, lakini hawakubahatika kuwa na makazi rasmi, hongereni sana,” alisema Rais Kikwete.
“Hongereni kwa kujituma na kucheza kwa ustadi,” alisema Rais na kuwaasa watoto hao “ongezeni bidii, nidhamu na mazoezi ya kutosha na hakika mtafanikiwa zaidi na kulibeba jina la Tanzania mbali zaidi ya hapa katika ulimwengu wa soka duniani, kwani hakuna kisichowezekana kama mtazingatia maelekezo, mafunzo, bidii na nidhamu ya yote mnayofanya.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment