Wameeleza hayo kupitia Kitabu cha Katiba Bora Tanzania walichokiandika, ambacho utangulizi wake umeandikwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala. Kitabu hicho kilikabidhiwa jana kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samiah Suluhu.
Pamoja na mambo mengine, kitabu hicho kinazungumzia Zanzibar kutoweza kukabiliana na changamoto za Muungano wa serikali tatu kiuchumi. Vile vile, kinasema Serikali ya Muungano katika muundo huo wa serikali tatu, itakuwa ombaomba.
Akikabidhi kitabu hicho, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Vyuo vya Kusini na Mashariki mwa Afrika (Esaurp), Profesa Ted Malyamkono, alisema baada ya kutafakari Muungano uliopo uliodumu kwa miaka 50, wameona ni vyema ubaki kuwa Muungano wa serikali mbili na maandalizi yafanyike kwenda serikali moja.
Taarifa ya Esaurp iliyotolewa sambamba na makabidhiano ya kitabu hicho mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, ilibainisha mambo manne ya kuzingatiwa wakati wa mjadala kuhusu idadi za serikali.
“Kwamba kila muundo wa serikali yoyote zitakuwepo changamoto, kwa hiyo serikali tatu hazitatui kero za serikali mbili. “Kwamba changamoto kubwa kuliko yote ni ya kiuchumi, wala si ya kisiasa kama inavyofikiriwa kati ya serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar. “Kwamba ieleweke kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 imevunja sehemu ya Katiba ya Muungano na serikali mbili, kama ilivyofahamika hapo awali.
“Kwamba duniani kote nchi ikiwa ndogo kiuchumi, eneo au hesabu ya watu, itaitegemea nchi nyingine, hasa ikiwa na vyanzo vya uchumi imara. Hii ni sababu kubwa ya Muungano na ndivyo ilivyo katika Umoja wa Ulaya (EU). Kwa hiyo Katiba itamke hivyo,” ilieleza taarifa ya wasomi hao.
Zanzibar
Kuhusu Zanzibar kushindwa kuhimili gharama za Serikali tatu, Profesa Nehemiah Osoro wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye alikuwepo wakati wa makabidhiano hayo na ameandika Sura ya Saba ya kitabu hicho, alisema gharama za serikali wanachama, zitaongezeka.
Kwa mujibu wa Profesa Osoro, ingawa mambo ya muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba, lakini hayo saba yaliyobakia ni sehemu kubwa ya gharama za Muungano na hivyo katika suala la gharama, kwa serikali ya Muungano zitapungua kwa asilimia tatu tu huku Zanzibar ikiathirika zaidi.
Katika sura aliyoandika, Profesa Osoro alisema “…katika muundo wa Muungano wa serikali tatu, nchi mbili huru (Tanganyika na Zanzibar), kila moja itahitaji fedha za ziada kwa ajili ya matumizi yake. “Chini ya Muungano uliopo, Zanzibar inapata fedha kutoka Serikali ya Muungano, wakati katika mfumo unaopendekezwa, italazimika kuongeza mapato ili kugharimia matumizi yake.
“Hili linawezekana kukabiliwa kwa kupunguza idadi ya wabunge na wizara …Halikadhalika Tanganyika itatumia fedha zake binafsi ili kugharamia matumizi yake. Katika mwelekeo huu, Zanzibar itaathirika zaidi kuliko Tanganyika,” ameeleza Profesa Osoro katika kitabu hicho.
Kuhusu serikali ya Muungano katika mfumo wa serikali tatu kuwa ombaomba, Profesa Osoro alisema kwa kuwa kutakuwa na Rais wa Muungano, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar; lakini Rais wa Muungano hatakuwa na rasilimali.
Profesa Osoro alisema katika kitabu hicho kuwa, “Tanzania Bara ni nchi kubwa na tajiri kwa madini na rasilimali nyingine za asili. Pamoja na usimamizi mzuri wa uchumi, ina uwezo wa kugharimia matumizi yake yote na kuchangia sehemu ya mapato yake katika Serikali ya Muungano.
“Kwa upande mwingine, Zanzibar ni nchi ndogo na idadi ya watu wasiopungua milioni na rasilimali chache. Kwa kifupi, mbali na utalii ni dhaifu sana kiuchumi. “Kama muundo wa serikali tatu utapitishwa, Zanzibar itabeba gharama zote za serikali yake, ambazo zitakuwa kubwa kuliko ilivyo sasa kutokana na kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu kutoka ngazi ya shirikisho kwenda ngazi ya nchi.
“Itatakiwa kugharimia mambo 15 ya Muungano ambayo yameondolewa kutoka katika mambo 22 ya sasa” ameeleza Profesa Osoro. Katika ufafanuzi zaidi, alisema serikali ya Muungano katika mfumo unaopendekezwa haitakuwa na rasilimali, lakini imepewa majukumu, ikiwemo kulipa majeshi.
Alisema kama serikali za nchi wanachama, zitakataa kuilipa serikali ya Muungano, kitakachotokea ni pamoja na jeshi kuchukua madaraka, jambo ambalo Makamu Mwenyekiti, Samia aliunga mkono.
Samia ashukuru
Baada ya kukabidhiwa kitabu hicho kilichoandikwa kwa Kiswahili na Kiingereza, pamoja na maelezo yake kwa ufupi kwa wasiopenda kusoma kurasa zote, Samia aliwashukuru wataalamu hao kwa kazi kubwa waliyoifanya.
“Sisi wanasiasa tulipewa siku 70 kutafuta Katiba mpya, tunashukuru kwa kazi mliyoifanya itatupa mwanga… mmefanya kazi kwa Taifa,” alisema Samia na kuongeza kuwa atawagawia wabunge wote wasome na kukitumia kujenga hoja.
Profesa Mukandala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Esaurp, katika utangulizi, ameandika; “Kitabu hiki kwa hakika kimetoka kwa wakati muafaka na kinaendana na mazingira yetu ya kisiasa. Profesa Geoffrey Mmari katika jalada la kitabu hicho, alisema; “Kitabu hiki pamoja na kongamano (la wasomi 100 waliokichambua) vitatoa mchango mkubwa katika kufikia uamuzi wa mwisho wa Bunge Maalumu la Katiba na hatimaye Watanzania, kuhusu Katiba Bora ya Tanzania.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment