Wednesday, 30 April 2014

WAJAWAZITO WALALAMIKIA KUOMBWA "KITU KIDOGO"

BAADHI ya kina mama hasa wajawazito wa vijiji vya Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini, wamewalalamikia wauguzi na wahudumu wa afya katika Kituo cha Afya Simambwe kwa kuwaomba ‘kitu kidogo’ wanapokwenda kituoni hapo kupata huduma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni baadhi ya wanawake kutoka vijiji vinavyohudumiwa na kituo hicho vya Usoha Njia panda, Shibolya, Simambwe, Garijembe, Ilembo Usafwa, Ngoha na Zunya walisema mjamzito amekuwa akiombwa kutoa sh 2,000 kila anapojifungulia nyumbani kwa dharura baada ya kushindwa kufika katika kituo hicho.
Mmoja wa wanawake aliyezungumza na mwandishi kwa masharti ya kutotajwa jina alisema ni jambo la kawaida wahudumu kuwaomba chochote wajawazito kituoni hapo.
“…unajua vijiji vingi vinavyohudumiwa na kituo hiki vipo mbali na miundombinu ya barabara si mizuri, yaani hakuna usafiri zaidi ya bodaboda ambazo lazima zitoke Simambwe…sasa kutokana na hali hii inapotokea mjamzito anajifungulia nyumbani akipeleka mtoto huyo kituo cha afya basi wanamuomba sh 2,000, haijulikani ya nini,” alisema.


Aidha, baadhi ya wanakijiji walikilalamikia kituo hicho kwa kitendo cha kudai muda wote hakina dawa huku wahudumu wakiwaelekeza kwenda kununua dawa katika maduka ya dawa.
“Muda wote ukienda kutibiwa utasikia hakuna dawa, tunaandikiwa kwenda kununua, tena wengine wanaelekeza hadi maduka ya kununua dawa hizo,” alisema mzee aliyejitambulisha kwa jina la Kalamwa.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe, Salome Mwaipopo,  alipinga kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi wa kituo hicho na kudai malalamiko kwa wanachi wanaohudumiwa na kituo hicho yamekuwa ni ya kawaida hasa wanapotembelewa na mgeni.
“Hakuna kitu kama hicho, unajua wakazi wengi wa vijiji hivi wamezoea kulalamika hasa wanapotembelewa na mgeni…hakuna anayewaomba fedha, mjamzito akijifungua nyumbani tunampokea bila masharti na kumpatia huduma anazostahili,” alisema Mwaipopo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!