TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliadhimisha vibaya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0.
Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Stars ilionekana kukosa maarifa ya kuidhibiti Burundi na hivyo kutoa nafasi ya wageni kutawala katika vipindi vyote.
Ikicheza mbele ya umati wa Watanzania ambao waliingia uwanjani bure baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza hivyo Stars ilijikuta ikitandikwa bao la kwanza katika dakika ya 45.
Bao hilo katika mechi hiyo ambayo Stars ilitumia wachezaji wengi chipukizi lilifungwa na Didier Kavumbangu baada ya kuunganisha pasi ya Ndarusanze Claude.
Stars ilizidi kufanya vibaya katika kipindi cha pili ambapo walijikuta wakifungwa mabao mengine mawili ndani ya dakika nne. Mshambuliaji wa Burundi anayecheza Simba Amisi Tambwe alifunga bao la pili katika dakika ya 56 kwa shuti kali ndani ya eneo la hatari baada ya kazi nzuri ya Kavumbangu.
Yussuf Ndikumana alifungia Burundi bao la tatu dakika ya 60 kwa shuti la umbali wa mita 50 baada ya kukutana na mpira akiwa katikati ya Uwanja kabla ya kumtungua kipa wa Stars Deo Munishi.
Baada ya bao hilo, Stars ilionekana kufurukuta kusaka bao lakini wachezaji wake wakiongozwa na Simon Msuva waliishia kukosa mabao. Ramadhani Singano alipata nafasi nzuri katika dakika ya 85 akipewa pasi na Msuva lakini alipiga mpira nje.
Kikosi cha Stars: Deo Munishi, Omar Kindamba/Himid Mao, Edward Peter, Aggrey Morris, Said Mourad, Said Juma/Jonas Mkude, Simon Msuva, Frank Domayo, Ayoub Lipati/Omar Nyenje, Mohamed Seif/Haroun Chanongo na Ramadhani Singano.
Burundi: Arthur Arakaza/Biha Omar, Kiza Fataki, Rugonumugabo Stephane, Issa Hakizimana, Rashid Leon, Yusuf Ndikumana/ Nahimana Chasil, Steve Nzigamasabo, Amisi Cedric, Didier Kavumbangu, Paschal Hakizimana/ Ndarusanze Claude na Amisi Tambwe/Shaaban Hussein.
HABARI LEO..
No comments:
Post a Comment