Matukio ya vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasi yamezidi kuongezeka nchini na kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), watu 34 waliuawa na watumishi wa vyombo hivyo katika nyakati tofauti.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana inaonyesha kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na sungusungu. Vyombo vingine vilivyotajwa katika matukio hayo ni polisi jamii na askari wa Wanyamapori. Pamoja na matukio hayo, pia askari wanane waliuawa na raia katika vurugu mbalimbali zilizohusisha pia kuvamiwa kwa vituo vinne vya polisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema matukio hayo yameongezeka kutokana na vyombo husika kutowachukulia hatua maofisa wake baada ya kutekeleza mauaji.
Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema jana kuwa baadhi ya askari wa jeshi hilo waliobainika kutekeleza vitendo hivyo walichukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu alisema watatumia ripoti hiyo kujirekebisha zaidi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za polisi.
Maeneo ya mauaji
Dk Bisimba alisema sehemu kubwa ya mauaji hayo yalitokea katika matukio baina ya askari na wananchi pia kupitia operesheni zilizotekelezwa na Serikali hususan Operesheni Tokomeza.
“Mambo makubwa matatu ndiyo yalikuwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu; Operesheni Tokomeza na Kimbunga pamoja na vurugu za gesi mkoani Mtwara,” alisema.
Alisema uvunjifu huo wa amani pia ulitokana na matamko ya viongozi wa Serikali ikiwemo kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni Agosti mwaka jana, kwamba wananchi wanaovunja amani wapigwe tu na vyombo vya dola.
Alisema mwaka 2013 kulikuwa na matukio ya kutisha ya mauaji kwa mfano, watu kujichukulia sheria mkononi na kuua wengine. Watu 1,669 waliuawa, ikiwa ni ongezeko la vifo 435 kutoka 1,234 mwaka 2012.
“Pia tulishuhudia aina mpya ya mauaji kama vile kumzika mtu akiwa hai kwa imani potofu za kishirikina, kuwapiga mawe na kuwachoma moto watuhumiwa... ni vitendo vya kutisha katika utoaji wa adhabu ambavyo vinavunja haki za binadamu. Pia kumekuwa na ugumu kwa upande wa polisi na waendesha mashtaka kufanya uchunguzi wa kina na kuwashtaki waliotekeleza vitendo hivyo.”
Ripoti hiyo ya kumi na moja tangu zilipoanza kutolewa mwaka 2002, pia imebainisha kuongezeka kwa vitendo vya kuwaua watu kutokana na imani za kishirikina. Watu 765 waliuawa mwaka jana ikilinganishwa na 630 mwaka 2012.
“Kati ya hao waliouawa wanawake walikuwa 505 na wanaume 260,” iliongeza ripoti hiyo ikisema mikoa iliyokumbwa zaidi na matukio hayo ni Geita, Mbeya, Shinyanga, Iringa, Tabora na Mwanza.
No comments:
Post a Comment