TANZANIA, leo inasherehekea miaka 50 ya Muungano wa kihistoria wa Tanganyika na Zanzibar, huku Rais Jakaya Kikwete akisema uko salama na kusisitiza hana shaka utaendelea kudumu na kwamba wale wachache wanaochukia na wanaotaka uvunjike wana lao jambo.
Akizungumza na wananchi kupitia vijana katika Ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni sehemu ya shamrashamara za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, alisema Watanzania wengi wanataka Muungano uendelee kuwepo na si uvunjike kama baadhi ya watu wachache wanavyotaka.
“Watanzania wengi wanataka changamoto na kero za Muungano kutatuliwa na sio kuvunjwa kwa Muungano na wanaotaka uvunjike wana lao jambo na sio wenzetu. Katika miaka 50 ya Muungano kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu wa pande zote mbili...hii ndio Tanzania ya miaka 50,” alisema na kuongeza kuwa Muungano uko salama na atakayeuchezea ‘atakiona cha mtema kuni’.
Rais alisema watu wasione ‘vinaelea, vimeundwa’ na ndiyo maana wengi wamekuwa wakijiuliza muungano wa Tanzania umewezaje kudumu na kuwataka Watanzania kuhakikisha Muungano unadumu kwa kuulinda na kustawi kwa sababu kudumu miaka 50 sio mafanikio madogo.
“Sina shaka Muungano utaendelea kudumu na kama viongozi tukileta chokochoko na kuudhoofisha Muungano na kuvunjika, tutakuwa tumewatendea dhambi kubwa wananchi, maana Muungano ukivunjika watakaoathirika watakuwa ni wananchi wakati viongozi watakuwa wanapita kwa raha bila tatizo,” alisema na kuongeza kuwa, kuna nchi nyingi duniani zilijaribu lakini zimeshindwa, huku nyingine zikiishia kuzungumzia kuungana kwenye kwenye meza ya mazungumzo.
Akizungumza kwa bashasha, alisema kumekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali kutokana na Muungano, jambo ambalo limekuwa ni la manufaa kwa Watanzania na kuongeza kuwa; kama ungekuwa hauna manufaa ungeshakufa siku nyingi.
Aliorodhesha baadhi ya faida za muungano huo kuwa ni kukua kwa uchumi, mafanikio katika elimu, afya na miundombinu. Hata hivyo alisema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto ambazo kutatuliwa kwake ni kwa kila Mtanzania kuwajibika kuboresha pale penye mafanikio na kuharakisha kuziondoa changamoto zilizopo.
Ukawa wamchefua Akizungumzia mchakato wa kutafuta Katiba mpya, Rais Kikwete dhamira yake ilikuwa kutoa fursa kwa Watanzania kujadili kwa kina, upana na kutambua yale ya muhimu yanayohitaji kuingizwa katika Katiba, ikiwa ni pamoja na kuondoa kero zilizobaki za Muungano.
Hata hivyo, Rais Kikwete alielezea kusikitishwa kwake na kitendo cha baadhi ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walioamua kususia bunge na kuwasihi warudi katika Bunge la Katiba ili kuendelea na mchakato wa kutunga Katiba mpya.
"Nawasihi warudi bungeni wakaendelee na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Wakati wa kwenda nje kwa wananchi bado, wanachotakiwa sasa ni kuwepo bungeni kujadili Rasimu na kutunga Katiba Mpya bungeni na sio kutembelea wananchi. Wasiokuwa bungeni hawawatendei haki wananchi. Wale miongoni mwa 201 ambao wametoka hawawatendei haki makundi yaliyowachagua,” alisema.
Rais Kikwete alisema wanachotakiwa ni kutunga Katiba mpya kisha wakimaliza kazi hiyo ndio watoke kwenda kushawishi wananchi kupigia kura mapendekezo yao, lakini kitendo cha kususia bunge kinatoa mwanya kwa watu kushuku dhamira ya wajumbe waliotoka.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete wajumbe wa Bunge la Katiba wana tatizo la uhusiano na ufumbuzi wake ni wao wenyewe na sio kwenda kwa wananchi na badala yake watumie Kamati ya Uongozi na Kamati ya Maridhiano kutatua matatizo yao badala ya kusumbua wananchi.
Alikemea matumizi ya lugha isiyokuwa na staha na matusi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wajumbe wa pande zote ndani ya bunge hilo na kuwataka kukaa na kukubaliana kwa hoja badala ya kutoleana lugha chafu na maneno yasiyofaa.
Rais Kikwete pia ameelezea kusikitishwa na kukasirishwa kwake na vitendo vya baadhi ya wajumbe wanapotukana waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa , hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Shekhe Abeid Amaan Karume.
“Inahuzunisha na kukasirisha sana Watanzania, pale wanapoona viongozi wa juu ambao ni waasisi wetu wanatukanwa, haikubaliki hata kidogo,hayo ni matumizi mabaya ya uhuru. Hawa ni mashujaa wetu, wasingejitoa mhanga siye tungekuwa wapi.
“Mwalimu Nyerere aliacha kazi yake ya ualimu yenye mshahara na kujitoa kwa ajili ya taifa hili. Yaani kwa sababu ya kutaka serikali tatu ndio utukane wazee?” alihoji.
Aliwashauri wajumbe wa pande zote mbili waache lugha za matusi na kejeli na kwamba wanaweza kutoa hoja zao bila kutumia lugha za maudhi, watumie mfumo waliojiwekea na waache kushindana na hatimaye waweze kupata Katiba itakayokuwa ya wote.
“Njia muafaka ni mzungumzo ya maridhiano, sio kufanyiana hila ila kushawishi na kujenga hoja kuvutia upande mwingine.Bado naamini Katiba mpya inawezekana kila mmoja akiwajibika kwa nafasi yake,” alisema.
Awali, Rais Kikwete alipokea maandamano ya vijana ambao walishiriki mbio katika kanda mbalimbali zilizopewa jina la Mbio za Uzalendo kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sixtus Mapunda akisoma hotuba ya vijana alisema maandamano hayo yalikuwa yana lengo la kuhamasisha vijana kudumisha muungano na kutumia fursa kujiletea maendeleo yao.
Mapunda alisema vijana wanaona nchi ina changamoto nyingi za kujiletea maendeleo na kundi linaloathirika ni vijana ambapo wanakabiliwa na changamoto za kukosa ajira, elimu, tatizo la dawa za kulevya, Ukimwi, mazingira magumu ya ushindani wa ajira na kwamba kinachotakiwa ni rasilimali fedha na rasilimali watu na sio kuongeza serikali ya tatu.
“Tunaomba fedha hizo za kuanzisha serikali ya tatu zipelekwe kwa ajili ya kuhudumia na kuondoa changamoto zinazowakabili vijana. Mbili zinatosha ya tatu ya nini,” alisema kwa niaba ya vijana wenzake na kuongeza kuwa Tanzania kwanza na mengine baadaye
No comments:
Post a Comment