VITENDO vya utekaji nyara watu vimeibuka jijini Dar es Salaam baada ya watu watano wenye asili ya kiarabu kutekwa wakiwemo watoto wanne wa familia moja na baadaye kuokolewa na polisi.
Watoto hao wenye umri wa miaka mitatu hadi 19 walitekwa katika mtaa wa Livingston, katika maeneo ya Kariakoo jijijini Dar es Salaam na baadaye kupatikana wakiwa wamefichwa kwenye hoteli mkoani Morogoro.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watoto hao walitekwa saa 8:00 mchana na baadaye kukutwa katika hoteli ya River View Lodge saa 10:00 alfajiri katika chumba namba A3.
Aliwataja watoto hao kuwa Sabrina Jamal (19), Faris Jamal (15), Zeana Mbaraka (14), Lela Mbaraka (3) wote wakazi wa Kariakoo.
Kova alisema polisi inamshikilia Shahir Haza (28) mfanyabiashara na mkazi wa Tandika kuhusika na tukio hilo.
Kova alisema katika tukio jingine polisi wamemwokoa Sameer Moledina (34) mfanyabiashara wa baiskeli na cherehani za jumla na mkazi wa Upanga baada ya kutekwa nyara na watu watatu waliojifanya polisi.
Watu hao walimtuhumu mfanyabiashara huyo kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kumwamuru kuingia katika gari Toyota Mark II nyeupe yenye namba za usajili T 726 AQG.
Alisema watekaji hao walimueleza kuwa wanampeleka katika kituo kikuu cha polisi lakini watekaji hao walibadili njia na walipofika Machinga Complex Ilala kulipokuwa na msongamano wa magari akabaini si kweli na kujitoa katika gari hilo kwa nguvu kwa kumsukuma jambazi mwingine.
Kova alibainisha kuwa wale majambazi walifyatua risasi na kumjeruhi mateka huyo katika goti na paja la mguu wa kushoto ambapo pia ilimjeruhi jambazi mwenzao.
Majambazi hao walikimbia ovyo na walipofika mtaa wa Songea, Ilala walipora gari namba T 726 CGD Toyota Duet yenye rangi kijani na kukimbia nalo na kuacha gari yao.
Alisema msako mkali unaendelea kuwakamata watekaji hao na majeruhi anaendelea vizuri na matibabu na mtuhumiwa aliyekamatwa atafikishwa mahakamani kwa kosa la utekaji.
No comments:
Post a Comment