WAJUMBE wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi na baadhi ya kundi la 201 waliosusa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, wameombwa kurudi bungeni kutengeneza Katiba kwani mchakato huo ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa na Watanzania wote.
Hayo yalisemwa jana bungeni, mjini hapa na Mjumbe wa Bunge hilo, Rashid Mtuta alipokuwa akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita.
Mjumbe huyo alisema wananchi wanawategemea wanasiasa kuwatetea na ikiwa hawafikirii kuwa mabilioni ya fedha yametumika tangu wakati wa kukusanya maoni hadi sasa wapo bungeni, kwao ni aibu.
“Nawaomba sana wenyeviti wenzangu wa vyama vya siasa na wafuasi wetu, turudi bungeni mabilioni ya fedha yametumika hadi sasa, sisi tukiingia mitini itakuwa ni jambo la ajabu sana…tutawapa Watanzania shida sana.
“Kufanya hivi ni kabisa tunawasaliti wananchi, nasema yote tunayosema bungeni itakuwa ni sema ya kinafiki au vinginevyo itakuwa kama ni sanaa sawasawa na Kaole Sanaa Group, hapa ni mahala pekee tunapoweza kutengeneza Katiba wananchi wanayoitaka,” alisema Mtuta.
Alisema pamoja na Bunge hilo kuendelea, hali ya hewa ndani humo haiko sawa kutokana na baadhi ya wajumbe wengine kutoka nje.
“Katika jambo hili hatuhitaji kuwa washabiki hata kidogo, tunahitaji kuwa makini kwa sababu ya mustakabali bora wa Taifa letu,” alisema.
Mtuta alisema akiwa Mwenyekiti wa chama cha siasa cha NRA pamoja na wanachama wenzake wanaamini kuwa katika mvutano na mgogoro njia pekee ni kukaa mezani na kuzungumza.
“Naomba niwaambie ndugu zangu, kwa vyoyote vile tukiwa kwenye jambo kama hili ni lazima kutakuwa na mvurugano, kwa sababu ya mawazo tu, hivyo basi ni vema sana tukatumia busara kila kundi likaheshimu kundi lingine, na mimi naamini katika makundi yote, yapo mawazo mazuri tu,” alisema.
Mtuta alisema iwapo wajumbe wote wataamua kugoma na kutoka nje ya mchakato huo watakuwa wamefanya usaliti kwa watanzania ambao tegemeo lao kubwa ni Katiba mpya.
Alisema kwa upande wake alikuwa akiunga mkono mawazo yanayotolewa na Ukawa na si kwa umoja huo tu bali hata kwa kundi lingine lolote linaloonekana lina mawazo mbadala yatakayoboresha katiba ya Watanzania.
Aidha, alimshauri Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kutumia lugha ya ukali kutoka na na lugha za kuudhi alizodai zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment