Wednesday, 9 April 2014
MKUCHIKA AKEMEA WANAOJICHUKULIA SHERIA MIKONONI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Amesema kukithiri kwa vitendo vya watu wanaojichukulia sheria mikononi, kumeiweka Tanzania katika nafasi ya 102 kati ya nchi 175 duniani katika suala zima la utawala bora.
Alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Transparency International na kutaka hatua kuchukuliwa kudhibiti wananchi wanaojichukulia sheria mkononi.
Waziri Mkuchika alisema hayo jana katika kikao cha Ushauri wa Mkoa (RCC) na kubainisha kuwa sasa hapa nchini kumekuwa jambo la kawaida mtu kujichukulia sheria mkononi na hata kufanya mauaji.
Alisema miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana kusikia mtu kuuawa lakini kwa miaka ya hivi karibuni suala hilo limekuwa kawaida.
“Ulaya watu wanalea babu zao ili wafikishe miaka 100 wafanye sherehe lakini hapa kwetu imekuwa ni tofauti watu wanaua sana vikongwe,” alisema.
Akizungumzia suala la rushwa alisema limekuwa tishio kubwa hapa nchini ambapo wananchi wamekuwa wakikosa huduma muhimu kama matibabu au haki zao kwenye vyombo vya sheria.
Waziri Mkuchika alisema hata rushwa kubwa imekuwa na athari sana kutokana na kuhusisha kiasi kikubwa cha fedha, hasa fedha za miradi ya serikali na mashirika ya umma.
“Rushwa ya aina hii inakuwepo wakati wa utoaji tenda (zabuni) na kusaini mikataba ya ujenzi na miundombinu hata manunuzi imekuwa na athari kubwa kiuchumi na huweza kuindisha sera na jitihada za kujenga na kuimarisha utawala bora,” alisema.
Alisema suala hilo limekuwa pia likisababisha watu kushindwa kulipa kodi kama inavyotakiwa.
“Tanzania mkwepa kodi ni shujaa na wananchi hawasikitiki kwa nini amekwepa kulipa kodi, lakini nchi za Ulaya kulipa kodi ni jambo la kawaida, na makampuni yanayofanya biashara yanatenga fedha kabisa kwa ajili ya kodi,” alisema.
Alisema asilimia 70 ya bajeti ya Tanzania inaishia kwenye manunuzi. Alisema madhara hayo yanaweza kuhatarisha usalama wa taifa kwani hata dawa zinakuwa hazipatikani na hata kusababisha wananchi kukosa imani na serikali yao na kujichukulia sheria mikononi.
Alisema vita dhidi ya rushwa ni ya kila moja lakini Watanzania wanaona aibu kufichua watu wanaokula rushwa.
Alisema takwimu kuhusiana na rushwa mkoa wa Dodoma katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2013 zinaonesha kuwa, jumla ya tuhuma 167 zilitolewa taarifa Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) .
Alsema idara za Serikali ndio zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya tuhuma 132, ikifuatiwa na mashirika ya umma 35, sekta binafsi tano, vyama vya siasa tano, watu binafsi saba.
Alisema kwa upande wa Idara za Serikali za Mitaa zinaongoza kwa kuwa na tuhuma 86 ikifuatiwa na idara ya polisi 17, Mahakama 16 na Elimu tuhuma nne.
Aidha tuhuma nyingine zilipatikana Idara ya afya mbili, Maliasili mbili, Kilimo mbili, Magereza, Maji na Ardhi zikiwa na tuhuma moja kwa kila moja.
Kwa upande wa mashirika ya umma, Mamlaka za Hifadhi za Taifa (Tanapa), inaongoza kwa kuwa na tuhuma sita, ikifuatiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) tuhuma tatu, Shirika la Umeme Tanesco tuhuma tatu, Vyuo Vikuu tuhuma tatu, Benki na Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (Duwasa) wakiwa na tuhuma moja kila moja.
Pia alisema kati ya tuhuma 86 zilizotolewa taarifa kutoka halmashauri, tuhuma 26 zilifunguliwa majalada, 18 zilifikishwa mahakamani, nane zilifikishwa kwa DPP na tano zilipata kibali cha mashitaka ambapo katika kesi saba Takukuru imeshinda na sasa kesi mpya 43 zimefunguliwa mahakamani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment