Tuesday, 29 April 2014
MCHINA AJINYONGA BAADA YA KUBORONGA KAZI!
Morogoro. Raia mmoja wa China ambaye ni mhandisi katika Kampuni ya Ujenzi ya China Railway Bureu 15 Group inayojenga Daraja la Mto Kilombero, Qin Bao Feng amekufa kwa kujinyonga kwa kile kinachodaiwa ni baada ya kuboronga katika kazi.
Ilielezwa kuwa Feng aliamua kujinyonga baada ya nguzo za daraja alilokuwa akilisimamia katika ujenzi huo, kusombwa na maji, jambo ambalo aliona kuwa limemvurugia kazi yake.
Baadhi ya watu waliokuwa jirani na kambi hiyo, walisema baada ya kuharibika kwa kazi hiyo, wahandisi wenzake kutoka China, walianza kumtenga hali iliyomfanya ajione kuwa mpweke na hatimaye kuchukua uamuzi huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita ndani ya kambi ya kampuni hiyo.
Alisema mwili wa marehumu ulikutwa ukining’inia kwenye dari ndani ya chumba alichokuwa analala na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.
Kamanda Paulo alisema baada ya kuchunguza mwili wa marehemu walikuta karatasi iliyokuwa imeandikwa ujumbe kwa lugha ya Kichina.
Alisema kwa kuwa hakuna mkalimani aliyekuwa jirani na eneo la tukio, polisi wanaendelea kumtafuta mtu wa kuutafsiri.
Alisema kwa sasa mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya St Francis iliyopo Kilakala, Morogoro.
Kivuko chazuiwa
Wakati huohuo, Halmashauri za Wilaya za Kilombero na Ulanga kwa pamoja zimeamua kusimamisha kwa muda usiojulikana matumizi ya Kivuko cha MV Kilombero Two kuvuka Mto Kilombero ambao umefurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kusimama kwa kivuko hicho kumesababisha baadhi ya wasafiri kukwama na wengine kulazimika kuvuka kwa kutumia mitumbwi.
Huduma pekee ya usafiri kwa sasa treni ya Tazara ambayo inafanya kazi mara moja kwa wiki.
Kamanda Paulo alisema uamuzi huo ulifikiwa Jumapili iliyopita baada ya kiwango cha maji kuongezeka.
Alisema ushauri wa kusitishwa kwa kivuko hicho ulitolewa na wataalamu wa vyombo vya usafiri wa majini na kwamba boti zinazotumia injini na mitumbwi ndizo zinazotumika kuvusha watu.
CHANZO:
MWANANCHI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment