MEYA wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutoa misada badala ya kutegemea ufadhili kutoka nje ya nchi.
Silaa alisema hayo kwenye hafla ya makabidhiano ya jengo la wagonjwa wa kifua kikuu lenye thamani ya sh milioni nane lililojengwa na mtaalamuwa tiba asilia, Dk. Abdallah Mandai, katika Zahanati ya Mongolandege, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kujifunza kutoka kwa Dk. Mandai kwa kufadhili miradi ya maendeleo ambayo itainufaisha jamii inayotuzunguka.
“Kituo hiki kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 200 hadi 250 wakati mwingine wagonjwa wanaokuja wanafika 900 kwa mwezi na kwa mwaka ni wagonjwa 100,000 hivyo msaada wa Dk. Mandai umekuja kwa wakati,” alisema meya huyo.
Kwa mujibu wa Silaa, msaada wa jengo hilo utapunguza msongamano wa wagonjwa kwenye zahanati hiyo na kuongeza kwa kuwahamasisha wakazi wa eneo la Mongolandege kudai haki ya kupata huduma bora za afya kupitia kamati za afya za eneo lao.
Kwa upande wake Dk. Mandai, amefikia hatua hiyo ili kurahisisha huduma kwa wagonjwa na kupunguza vifo hasa vya mama na mtoto.
TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment