Wednesday, 30 April 2014

HABARI ZAIDI JUU YA MAJAMBAZI WALIOUA ASKARI POLISI URAMBO TABORA


Baadhi ya askari Polisi wakiutoa mwili wa askari Polisi kwenye Wodi namba moja aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi huko katika Tarafa ya Ussoke wilayani Urambo askari huyo aliyefahamika kwa namba F.5179 PC JUMANNE,walipigwa risasi wakiwa na askari mwenzake ambaye pia alifariki papo hapo namba G.3388 PC SHABAN.


ASKARI Polisi wawili kutoka Tarafa ya Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora, wameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi. Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan
Kaganda, alisema mauaji hayo yamefanyika juzi saa 2: 30 usiku katika
kijiji cha Usoke wilayani Urambo.

Kamanda Kaganda aliwataja askari waliouawa kuwa ni PC Shabani,
mwenye namba G 3388 ambaye alikufa papo hapo baada ya kupigwa
risasi na majambazi hao.
Mwingine ni PC Jumanne mwenye namba F.5179, aliyejeruhiwa tumboni
na baadaye kufa jana saa 4 asubuhi, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda huyo alisema majambazi hao walikuwa watatu na kabla ya mauaji hayo, walivamia nyumbani
kwa mfanyabiashara Ibrahim Mohamed, ambaye ni mkazi wa Usoke na kupora fedha taslimu Sh 1,200,000.
Mbali na uporaji wa fedha, pia walipora vocha za simu aina mbalimbali zenye thamani ya Sh 120,000 ambapo baada ya askari
hao kupata taarifa ya uhalifu huo, walienda eneo la tukio kutoa msaada zaidi.

Kamanda huyo wa Polisi, alifafanua kuwa askari hao wakiwa mita chache kabla ya kufika katika eneo la tukio, walikutana na
majambazi hao na kuanza kuwafyatulia risasi kwa kasi na kumuua PC Shaabani.
“Ndugu zangu waandishi wa habari hili ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Polisi, lakini naapa kuwasaka hadi kuwakamata wakiwa
hai au wafu...tumechoka na uhalifu huu,” alisema Kaganda.

Kamanda Kaganda alisema kabla ya mauaji ya askari hao, majambazi hao walifyatua risasi hovyo hewani kwa lengo la kuwatisha
raia ambapo maganda 25 ya risasi aina ya SMG na SAR yameokotwa katika eneo la tukio.
Kutokana na mauaji hayo, Polisi mkoani Tabora wanaendesha msako mkali usiku na mchana, ambapo tayari hadi sasa watu
watano wametiwa mbaroni na Polisi wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda Kaganda alitoa mwito kwa wananchi mkoani Tabora, kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa
zitakazowezesha kuwabaini majambazi hao.

Akizungumzia mauaji hayo jana katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alitoa pole kwa wananchi wote waliofiwa na ndugu zao.
Alisema Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali wa majambazi hao ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani na kuwaomba
wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa aina yeyote ile, ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!