Watanzania wengi hasa vijana na hata ambao ni watu wazima hawajui na hawajapata nafasi ya kujiuliza kwanini Muungano wetu una serikali mbili na siyo tatu na kwanini serikali hizo ziko jinsi zilivyo.
Kutokana na kutojua hili wengi hufanya haraka na kusema “tuwe na serikali tatu” bila kujiuliza kama kufanya hivyo kutatua tatizo au la au kutaongeza tu tatizo. Nyerere aliwajibu wale wenye kuhoji haya kwa kuwapa historia kidogo ya mfumo wa Muungano. Kwa kutumia hoja za kimantiki na kiufundi wa maneno kuonesha kuwa Muungano wa Tanzania ndio nchi pekee katika Afrika iliyoundwa na Wananchi wenyewe.
Tanzania siyo zao la mipaka ya ukoloni au matokeo ya Mkutano wa Berlin wa 1884-1885 kama zilivyo nchi karibu zote za kiafrika. Nyerere alijenga hoja kuwa Watanzania wasiwe dhaifu kukumbatia kilichoundwa na mkoloni kuwa ni chao halafu walichounda wao wenyewe kukibeza na kujaribu kukivunja. Siyo hivyo tu, alishangaa kwanini watu waone kilichoundwa na mkoloni bila kura ya maoni ya waliotawaliwa au kwa hiari ya wananchi kuwa ni halali lakini kilichoundwa na wananchi wenyewe kwa makubaliano ya wananchi bila ya kura ya maoni kuwa ni haramu?
CHANZO: JMF
No comments:
Post a Comment