Kundi la wezi wanaotumia funguo bandia kufungua milango ya vyumba katika nyumba za kulala wageni limevamia mjini Dodoma likilenga wageni waliopanga katika nyumba mbalimbali.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema mwandishi wa habari wa Kampuni ya The Guardian, David Mtey amekuwa mtu wa pili kuibiwa mali zake akiwa katika nyumba moja ya kulala wageni.
Mwandishi huyo ambaye ni miongoni mwa wanahabari wanaoripoti habari za Bunge Maalumu la Katiba, aliibiwa kompyuta mpakato na pochi yenye fedha.
Habari zilisema wakati mwandishi huyo alipotoka katika chumba chake na kwenda kupata mahitaji binafsi, watu wasiojulikana walifungua chumba hicho kwa kutumia funguo bandia na kuiba vitu hivyo.
Hata hivyo, kutokana na haraka waliokuwa nao, watu hao waliacha fuko lenye funguo nyingi bandia zinazotumika katika kufungulia milango ya hoteli na nyumba za kulala wageni.
Wiki iliyopita pia katika nyumba moja ya kulala wageni, mtu mmoja alikamatwa na kupewa kibano baada ya kuingia katika chumba cha mteja mmoja na kuiba kiasi cha Sh300,000.
“Huyo mteja alikuwa ametoka kidogo aliporudi alishangaa kukuta mtu akiwa ndani ya chumba chake na alijaribu kutoroka lakini akazingirwa na wananchi wanaoishi jirani,” alidokeza mwanahabari mmoja.
Tukio la kuibiwa kwa mwandishi huyo wa Kampuni ya The Guardian ni la tatu kuwakumba wanahabari kwani Novemba mwaka jana, waliibiwa kwa staili hiyo.
Miongoni mwa waandishi hao ni Bakari Kimwaga ambaye aliibiwa kompyuta mpakato katika nyumba ya kulala wageni na mwizi alikamatwa lakini haijulikani kesi hiyo ilimalizika vipi.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alikataa kuthibitisha wala kukanusha juu ya kuwepo wezi hao
MWANANCHI..
No comments:
Post a Comment