Friday, 28 March 2014

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUAGA MWILI WA MAREHEMU TUPPA


Viongozi Dini wakiongoza ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na hapo awali aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,aliefariki ghafa siku kadhaa zilizopita.

Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na hapo awali aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,aliefariki ghafa siku kadhaa zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu wa Bunge),Mh. William Lukuvi akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mh. Rehema Nchimbi akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Jeneza lenye mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara likiwa uwanja wa Nyerere mjini Dodoma wakati wa ibada ya kuuaga.
Viongozi mbali mbali wa Vyama na Serikali wakiwa kwenye Ibada ya Kuaga mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.





WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi mbalimbali na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mara ambaye alifariki dunia ghafla Machi 25, 2014 akiwa ziarani wilayani Tarime.

Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu John Gabriel Tuppa kwa wakazi wa mji wa Dodoma ilifanyika leo mchana (Ijumaa, Machi 28, 2014) kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako ibada ya kumwombea marehemu ilifanyika. Baadaye mchana, mwili wake ulisafirishwa kwenda wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kwa mazishi.

Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Padri Chesco Msaga ambaye aliongoza ibada hiyo, alisema Mungu aliwaumba wanadamu ili wampende na wamtumikie na kwamba marehemu Tuppa alilitimiza jambo hilo vilivyo.

Alisema wakati wa uhai wake, Bw. Tuppa alipenda haki na popote alipokwenda alitetea haki za wanyonge. “Sote ni mashahidi wa jinsi alivyopenda watu na jinsi alivyowatumikia watu. Alikuwa mnyenyekevu, aliwasikiliza wengine na alithamini michango ya wengine. Na sisi tunapaswa kuiga hilo,” alisema.

Naye Dk. Right Mmbaga, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Baraza la Wazee la Dodoma Mjini alisema: “Wale watumishi ambao bado wako kazini na walipata nafasi ya kufanya kazi na Bw. Tuppa, wajifunze kutoka kwake na wafuate nyayo zake kama njia ya kumuenzi.”

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba, akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, alisema Chama cha Mapinduzi kimempoteza kamisaa makini sana aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Bw. William Lukuvi aliwaasa wakazi wa Dodoma kuenzi mambo ambayo Bw. Tuppa aliwafanyia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma hata kama walikuwa hawayaoni.

“Alikuwa na upeo wa kufanya kazi kwa spidi lakini kwa utulivu. Wakati tumeanza naye kazi hapa Dodoma mwaka 2006, kulikuwa na shule sita tu za sekondari lakini katika kipindi cha miaka miwili alifanikisha kusimamia ujenzi wa shule za sekondari 30,” alisema Bw. Lukuvi ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Makanisa ya mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Yohana Masinga alisema viongozi hawajui kwamba wakishateuliwa, wao ni watumishi wa Mungu kwa sababu wanawaongoza watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu..

Akinukuu neno la Mungu kutoka kitabu cha Waebrania sura ya 13 aya ya 7, linalosema wakumbukeni waliokuwa wakiwaongoza, ichunguzeni miisho ya mwenendo wao na iigeni imani yao, Askofu Masinga aliwataka wote waige mfano wa utendaji kazi wa Bw. Tuppa.

“John Tuppa alikuwa ni mtendaji na kanisa limempoteza mtu makini. Ninawaomba viongozi wa nchi hii waige mfano wa John Tuppa. John Tuppa awe ni mfano kwao, na wafanye hivyo kwa ukombozi wa nchi yetu,” alisema.

Bw. Tuppa anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi, Machi 29, 2014) wilayani Kilosa. Alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara  mwaka 2011. Ameacha mke na watoto watano.

Picha kwa hisani ya Isa Michuzi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!