Serikali ya Kenya imewaagiza wakimbizi wote wanaoishi nje ya kambi za Kakuma na Dadaab kurudi katika kambi hizo haraka iwezekanavyo.
Halkadhalika imetangaza kusitisha usajili wa wakimbizi zaidi katika maeneo ya mijini ikiwemo Nairobi, Mombasa, Malindi, Isiolo na Nakuru.
Wakenya wametakiwa kuripoti kwa polisi wakimbizi wowote watakaosalia maeneo na mijini pamoja na raia wa kigeni wasio na vibali halali vya kuishi nyumbani.Haya ni wakati maafisa mia tano zaidi wa kikosi cha usalama wametumwa katika mji mkuu Nairobi na Mombasa, ambapo watu sita waliuawa walipofyatuliwa risasi wakiwa kanisani na watu waliojihami kwa silaha.
Waziri wa usalama nchini humo Joseph Ole Lenku amesema kuwa mkimbizi yeyote atakayepatikana nje ya kambi atakabiliwa vilivyo na polisi.
Shambulizi lililotokea mjini Mombasa siku ya Jumapili lilitokea huku kundi la kigaidi la Al Shabaab likiendelea kutishia usalama wa nchi hiyo.
Hii ni hata baada ya usalama kuimarishwa nchini humo.
Hata hivyo hakuna mtu au kundi lolote lililokiri kufanya shambulizi hilo dhidi ya waumini wa kanisani ambapo watu sita waliuawa.
Kundi la wanamgambo la Al Shabaab limetoa uonyo kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa wanajeshi wake nchini Somalia, basi itaendelea kushambuliwa.
Shambulizi la kanisani mjini Mombasa, lilitokea baada ya polisi kuwakamata washukiwa wawili walipokuwa wamejihami kwa mabomu mawili na vilipuzi vinginevyo ambayo maafisa wa usalama walisema kuwa yalikuwa na uwezo wa kuangusha jengo kubwa.
Waziri Lenku amesema kuwa polisi zaidi 500 watashika doria mjini Nairobi na Mombasa.
No comments:
Post a Comment