Thursday, 6 March 2014

JE WAJUA?KUSITISHWA KWA 'AFRIKANAIZESHENI' KULISABABISHA KUASI KWA JESHI LA TANGANYIKA MWAKA 1964 FUNGATE YA UHURU NA MADARAKA KWA WAZAWA





USIKU wa kuamkia Januari 21, 1964, Jeshi la Tanganyika liliasi na kushikilia serikali kwa muda, tukio ambalo aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilielezea kuwa ni “siku ya aibu sana kwa Taifa”.



Wakati jeshi hilo likiasi; siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo hiyo. Maasi yote ya nchi tatu hizo yalizimwa na majeshi ya Uingereza siku moja na wakati huo huo. Kwa Tanganyika, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar, Januari 12, 1964.

Disemba 9, 1961 Tanganyika ilipata Uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, Mara baada ya Uhuru wake Tanganyika ilirithi karibu kila taasisi ya Umma iliyokuwa chini ya Serikali ya Kikoloni, likiwemo Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, Desemba 9, 1961, Jeshi hilo likijulikana kama “Kings African Rifles” – (K. A. R) na baadaye kuitwa “Tanganyika Rifles” (TR).

Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake, zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru ukijulikana zaidi kama 'AFRICANIZATION'.

Uhuru ulikuja na mambo yake, ikiwa ni pamoja na hamasa ya wananchi kutaka kuona nafasi zote za utawala na uongozi zinashikwa na wazalendo kuashiria “uhuru” wa kweli na kukomesha kupuuzwa na kudhalilishwa kwa Mwafrika.

Hatua ya Mwalimu Nyerere ya kuomba na kukubaliwa na Malkia wa Uingereza kumwongezea Gavana wa Kizungu muda kubakia nchini kusimamia Serikali, ilionekana kwa wanasiasa wenye “siasa moto” kuwa ilipingana na kauli yake juu ya Watanganyika kujitawala na kusimamia mambo yao wenyewe; walitaka Gavana aondoke na Tanganyika iwe Jamhuri na nafasi za kazi zote muhimu zishikwe na Waafrika. Lakini kwa Mwalimu, mpango wowote wa kuwapa kazi za madaraka Watanganyika weusi pekee, na kutowaruhusu wageni wa rangi zingine kujiunga na TANU, ulikuwa aina ya ubaguzi, akataka yeyote asiyeamini usawa wa binadamu.

Hatua hiyo ilipata ukinzani mkubwa mno, Kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli, Ndugu Christopher Kassanga Tumbo, alitishia kuitisha mgomo nchi nzima kupinga kauli ya Nyerere, na akitoa hoja bungeni, aliwaita watumishi wa Serikali wa Kizungu “Mamluki – Askari wa kukodiwa”. Kassanga Tumbo hakudumu nchini, kwani Aprili 1962 alipelekwa London kuwa Balozi mpya wa Tanganyika kufanya Serikali ipumue.

Hata hivyo, kwa jeuri kubwa, mwezi Agosti 1962, Tumbo alijiuzulu kazi na kurejea nchini na kuanzisha Chama cha “People’s Democratic Party” (PDP) kupambana na Nyerere, ingawaje Chama hicho hakikudumu zaidi ya Uchaguzi Mkuu wa Novemba 1962, na yeye akaenda Mombasa kufanya kazi ya uandishi wa habari.

Mpinzani mwingine mkubwa wa Nyerere na Kiongozi wa Chama cha “African National Congress” (ANC), Zuberi Mtemvu, alisema Nyerere alitaka kuleta “ukoloni mambo leo” Tanganyika na katika nchi changa za Afrika; na hivyo Mei, 1962 alitangaza kile kilichoitwa “Mpango moto sana” ili kupata Serikali ya Waafrika watupu ndani ya mwaka mmoja.

Nyerere hakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua haraka hivyo, kama pia ambavyo Waziri wake wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Clement George Kahama, hakuwa na ujasiri wa kuwatimua Waingereza katika nafasi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.

Yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU), kwamba Nyerere alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni, na hivyo kwamba “uhuru” haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika. Na ukatungwa uzushi kuwa baba wa Mzalendo Amir Jamal, Mzee Habib Jamal amemuhonga Mwalimu Nyerere ili mwanaye ateuliwe katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Tanganyika.

Hamasa ya Watanganyika kutaka nafasi zote za uongozi na utawala zichukuliwe na Wantanganyika weusi, na hatua ya Nyerere kuita hatua hiyo ni “ubaguzi mbaya kuliko ule wa Verwood wa Afrika Kusini”, ulikiweka Chama cha TANU na Nyerere mwenyewe njia panda kufuatia malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya TANU, kwamba alikuwa anairudisha Tanganyika kwenye ukoloni mpya hivi kwamba uhuru kwa Watanganyika haukuwa na maana tena kwao. Kikao hicho cha dharura cha NEC, kiliitishwa na Wajumbe mahsusi kujadili kauli hiyo ya Nyerere.

Gazeti la TANU la “Uhuru”, lilikuwa limeanza kutumia lugha kali kali za kibaguzi kwa chukizo la Nyerere, likiwaita Wahindi nchini “Nyoka”, na Maafisa wa Kiingereza waliosalia “Manabii wa ukoloni".



Pichani ni Rais wa Chama cha TANU Ndugu Julius Kambarage Nyerere (Katikati) akifurahia jambo na Wazalendo wenzie Amir Habib Jamal (Kulia) na Derick Breyson, Amir Habib Jamal na Derick Breyson ni Miongoni mwa Mawaziri waliobaguliwa kwa sababu ya kulazimishwa kutekelezwa dhana ya 'Afrikanaizesheni'.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!