Katika makala zangu nilizowahi kuandika, nimeibua mawazo mengi kutoka kwa wasomaji wangu ambao wananiletea ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii kwa mfano Facebook.
“Mimi nilisoma Kiswahili hadi kidato cha sita na nimekuwa nikifuatilia uandishi wako kuhusu ufasaha wa lugha ya Kiswahili. Nilitamani sana siku moja ungeweza kuinusuru lugha hii ili itumike kama lugha ya kufundishia nyanja zote za elimu. Sasa niko Chuo Kikuu cha SUA, nachukua digrii ya Maendeleo ya Jamii. Huko ndiko nitaenda kufanya kazi na wanakijiji ambao wengi wao hawajui Kiingereza. Inaniuma sana kwa kuwa nakiona Kiswahili kinashushwa hadhi na wakati huo huo wananchi wananyimwa haki ya msingi ya kuletewa maendeleo sahihi kwani kuna mambo nitashindwa kuwasaidia. Je, nifanyeje ?
Katika hoja hii liko suala la kukifanya Kiswahili kiweze kutumika kama lugha ya kifundishia katika mfumo mzima wa elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu.
Wazo hili si geni kwa wadau wa Kiswahili kwani utafiti uliofanyika mwaka 1978 na wataalamu wa Idara ya Kiswahilli na Sanaa za Maonyesho zote za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliweka wazi suala hili. Ilidhihirisha kuwa walimu na hata viongozi wa Wizara ya Elimu na Utamaduni wakati huo walikubaliana na hoja hiyo lakini ilikwamishwa na kigogo mmoja.
Watafiti walibaini baada ya kuwahoji walimu, wakuu wa shule za sekondari na vyuo vya ualimu na pia wakufunzi kuwa Kiswahili kikitumika kama lugha ya kufundishia katika shule za sekondari uelewa wa dhana za sayansi, hisabati na masomo ya sanaa yangeleweka vizuri zaidi kuliko kutumia Kiingereza ambacho wanafunzi wengi hawana misingi imara.
Watafiti walibaini pia kwamba inawabidi walimu wafundishe kidato cha kwanza kwa Kiswahili, baadhi ya dhana ngeni na baadaye kuzitafsiri kwa Kiswahili ili hatimaye wanafunzi waweze kufuatilia kwa karibu masomo yao kwenye vitabu. Kufundisha kwa njia ya tafsiri kunarudisha nyuma mpangilio wa ufundishaji kwani walimu inawawia vigumu kumaliza mpango wa kazi (Scheme of work) kama walivyoelekezwa na Wizara ya Elimu.
Kutokana na uelewa ndogo wa lugha ya Kiingereza, ziko baadhi ya shule za binafsi kama vile seminari huwafanya wanafunzi wasome kidato cha kwanza kwa miaka miwili. Lengo ni kuwajenga katika fasihi na sarufi ya Kiingereza ili kuwawezesha kuyaelewa masomo ya kidato cha pili na kuendelea.
Shule nyingine hutumia miezi miwili hadi mitatu kuwaandaa wanafunzi kabla ya kuanza mihutasari ya masomo yao. Hii inajulikana kama ‘Pre Form One’.
Tutaweza kuondokana na mkanganyiko huu katika shule za sekondari kwa kufanya uamuzi wa busara na kuthubutu kutumia Kiswahili kufundishia masomo yote kwa Kiswahili. Hii ina maana kuwa Kiingereza kifundishwe kama somo kuanzia shule za msingi, sekondari na elimu ya juu.
Kabla uamuzi huu haujafanyika yatakiwa kuwa na maandalizi makubwa. Kwanza ni kulipatia Baraza la Kiswahili fedha na utaalamu wa kutosha wa kuandaa istilahi za masomo kama Fizikia, Kemia, Biolojia, Hisabati, Jiografia, Uchumi na Historia. Wataalamu wa masomo haya washirikishwe kwa kila somo ili kupata visawe vinavyoeleweka kulingana na misingi ya Kiswahili.
Eneo la pili ni utayarishaji wa makala na vitini vya kufundishia na baada ya kupata mrejesho kutoka kwa walimu wa watumiaji wengine, kama wachapishaji ndipo vitabu vitayarishwe.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment