Marehemu waziri wa Fedha wa Tanzania, Dokta William Mgimwa
Kifo cha Mgimwa kinafanya wizara tano kukosa mawaziri baada ya wengine wanne kufukuzwa kutokana na kashfa iliyowakumba viongozi na watendaji wa wizara hizo.
Baadhi walikwenda kinyume na utaratibu wakati wa Opereheni ya Tokomeza Majangili iliyolenga kuwanusuru wanyama walio katika hatari ya kutoweka kama vile Tembo na Faru kutokana na uwindaji haramu unaochochewa na kushamiri kwa biashara haramu ya vipusa na pembe za ndovu katika nchi za Asia.
Mawaziri waliokumbwa na kadhia hiyo ni wale ambao wizara zao zilihusika kwa namna moja au nyingine katika kusimamia na kutekeleza operesheni ya kupambana na majangili katika hifadhi za taifa, ambapo waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alilazimika kujiuzulu, ili kuwajibika kisiasa.
Wengine ni waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dokta Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dokta Mathayo David Mathayo.
Katika operesheni hiyo kulitolewa malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu, uliosababisha baadhi ya watu katika maeneo ya Hifadhi za Taifa kuuawa, kupata ulemavu na hata mifugo kuuawa.
Malalamiko hayo yalilisukuma Bunge la Tanzania kuunda kamati ya kuchunguza madai hayo ya wananchi na kisha kuwasilisha ripoti iliyowatuhumu watekelezaji wa operesheni hiyo kwenda kinyume na maagizo ya utekelezaji wake.
Baada ya ripoti hiyo Rais Jakaya Kikwete aliafiki hoja za wabunge na kuwafukuza kazi mawaziri hao.
Katibu Mkuu Kiongozi wa serikali ya Tanzania, Balozi Ombeni Sefue alitangaza kifo cha waziri Mgimwa kuwa kilitokea Jumatano asubuhi saa 5:20 kwa saa za Afrika Mashariki.
Mipango ya kurudisha nyumbani mwili wa marehemu inafanywa na serikali kwa kushirikiana na familia yake
Mipango ya kurudisha nyumbani mwili wa marehemu inafanywa na serikali kwa kushirikiana na familia yake
BBC SWAHILI.
No comments:
Post a Comment