Thursday, 9 January 2014

SUMAKU MAALUM YANASA WEZI WA NONDO JIJINI

Nondo


SUMAKU maalumu zilizofungwa kwenye lango la kuingia kwenye mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, zimesaidia kukamata wezi wa nondo na misumari.
“Wizi upo, lakini tumekabiliana nao, ilibainika kuwapo watu wa nje wanaojichomeka kwenye kazi na kuiba, walikuwa wanajivisha vipande vya nondo maungoni na kujifunga, wengine kutumia nywele ndefu kuficha zaidi ya nusu kilo ya misumari. “Tulifunga sumaku maeneo ya kutokea na kuingia na baadhi walivutwa nayo kutokana na vyuma walivyoficha maungoni na kukamatwa kirahisi sana, sasa wizi umepungua,” amebainisha Meneja Mradi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Karim Mataka.



Alikuwa akizungumza katika ziara ya kawaida ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Musa Iyombe, kuelezea changamoto zinazoukabili mradi huo.
Alisema hiyo ni moja ya changamoto kati ya nyingine ikiwamo ya kukuta uwazi, mapango na mikondo ya maji chini ya kina cha bahari, na kulazimu baadhi ya nguzo ikiwamo namba nane, kuongezwa urefu.
“Iliwalazimu wajenzi waongeze kina, katika ujenzi walifika kwenye kina cha meta 64 kilichokusudiwa, lakini kwa baadhi ya nguzo kulikuwa na mikondo ya maji chini ya bahari na ilibidi ziteremshwe zaidi hadi nyingine meta 84 ili kuzuia daraja kuleta madhara baadaye, changamoto hii haikuwa ndogo, kwa kila eneo ilitumia siku si chini ya 15 kupata ufumbuzi na kumaliza tatizo, sasa kazi inaendelea,” alisema Mataka.
Changamoto hizo kwa mujibu wa Mataka zilifanya muda wa kukamilika kwa daraja hilo kuongezeka, hali ambayo pia ilizungumzwa na Katibu Mkuu Iyombe katika ziara hiyo ya jana.
Alisema muda wa kumaliza ujenzi wa daraja hilo, utaongezeka kwa miezi sita kutokana na changamoto hizo. Iyombe alisema awali ujenzi ulipangwa kukamilika Januari mwakani, lakini kutokana na changamoto hizo na nyingine zinazofanyiwa kazi hivi sasa, utakamilika Julai.
“Hii ni ziara ya kawaida ya ukaguzi wa mradi huu mkubwa, mradi unaendelea vizuri lakini zipo changamoto nyingine walikutana nazo,” alisema Iyombe.
Pamoja na changamoto hiyo, pia alisema changamoto za awali zilizoripotiwa kuwa kikwazo kwa mradi huo, ni wakazi wanne wa Vijibweni kugomea fidia na kupisha ujenzi wa barabara, nazo zimefanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa na Serikali itawalipa wahusika kulingana na bei ya soko na wakigomea malipo hayo, nguvu zitatumika.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakamilisha tathmini ya fidia ya malipo yao.
Kuhusu kero inayolalamikiwa na mkandarasi wa ujenzi kwa baadhi ya wanajeshi kulazimisha kupita kwenye daraja la muda wakati ujenzi ukiendelea, Iyombe alisema anafanya mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili kumaliza tatizo hilo.
Mataka alisema changamoto ya kukuta uwazi, mapango na mikondo ya maji chini ya kina cha bahari, ililazimu nguzo namba nane, kuongezwa urefu wa meta 84 tofauti na 64 za awali.
Mhandisi wa Daraja wa Kampuni ya Arab Consulting Engineering (ACE) ambao ni washauri wa ujenzi wa mradi huo, Mohamed Abdel Bary alisema ujenzi unaendelea vizuri lakini mikondo ya maji iliwapotezea muda ingawa wamekabiliana nayo.
Alisema kwa daraja pekee, mradi umekamilika kwa asilimia zaidi ya 40. Baada ya kukagua daraja hilo lenye urefu wa meta 680, na barabara yenye urefu wa kilometa 2.5; kilometa moja kwa upande wa kutoka darajani hadi Kurasini na kilometa 1.5 Kigamboni, Katibu Mkuu alitembelea barabara ya Nelson Mandela, eneo la Shimo la Udongo na kuagiza Wakala wa Barabara (Tanroad) kuvunja eneo la jengo la Hoteli ya Lemira iliyo barabarani.
Aidha, alizungumza na mamalishe wanaofanya biashara eneo hilo wasitishe kuuza chakula kuanzia leo ili kazi ya mradi ya kuhamisha mabomba ya gesi katika eneo hilo ifanyike ili barabara ya juu itakayounganisha daraja na barabara ya Mandela iweze kujengwa kwa ufanisi.
Mradi wa daraja la Kigamboni unagharimu Sh bilioni 214.6; asilimia 60 zikitolewa na NSSF na asilimia 40 na Serikali. Litakapokamilika, litakuwa na uwezo wa kubeba uzito wa tani 50.
Mkandarasi Mjezi wa Daraja hilo ni Kampuni ya China ya Major Bridge kwa ushirikiano na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!