Friday, 3 January 2014

MWILI WA MGIMWA KUWASILI KESHO MCHANA

Marehemu Dk William Mgimwa
Marehemu Dk William Mgimwa.




MWILI wa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa unatarajiwa kuwasili nchini kesho mchana kwa ndege ya Afrika Kusini.
Utaagwa keshokutwa katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Jumatatu kwenda kuzikwa kijijini kwake Magunga, Wilaya ya Iringa Vijijini.
Akitoa taarifa kuhusu mazishi, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi Kitaifa, William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge) alisema mwili utapokewa kesho saa 7 Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Terminal II.
Lukuvi alisema baada ya hapo, utapelekwa nyumbani kwake Mikocheni B na saa 11 jioni utapelekwa katika Hospitali ya Lugalo utakapolala.
Alisema Jumapili saa 3:00 hadi 4:00 kutakuwa na chakula nyumbani kwa marehemu, kisha saa 4:30 mwili wa marehemu utawasili nyumbani kwake kutoka hospitalini kabla ya kupelekwa Karimjee kwa ajili ya ibada na heshima za mwisho.
Baada ya kuagwa, utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Termina II na kusafirishwa kwa ndege ya Serikali kwenda mkoani Iringa kwa maziko.
Inatarajiwa saa 10:00 alasiri mwili utawasili katika Kiwanja cha Ndege cha Nduli na kupokewa na wananchi wa mkoa huo, ambako mipango ya maziko inafanywa na Kamati ya Mkoa inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Dk Christine Ishengoma. Utaagwa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, ambako Dk Mgimwa inaelezwa alifanyia kazi kwa muda mrefu.
“Baadaye saa 11:30 jioni (Jumapili) mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea kijijini kwake, Magunga utakapolala na siku inayofuata yaani Jumatatu saa sita mchana shughuli za maziko zitaanza kijijini hapo,” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Kamati ya Mazisho imejumuisha wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Afya, Bunge, Ikulu, Mambo ya Nje na Ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kuhusu tatizo lililosababisha kifo, Waziri Lukuvi alisema zitaelezwa katika ukumbi wa Karimjee wakati wa shughuli za kumuaga. Wakati huo huo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na kifo cha Waziri Mgimwa.
Katika salamu zake, Dk Shein alisema daima atakumbukwa kutokana na utumishi wake uliotukuka kwa Serikali na wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpenda kazi, mzalendo na mtu mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema Dk Shein kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!