Kituo cha kuvumbua vipaji cha Mkubwa na Wanawe cha Temeke, jijini Dar es Salaam kinatarajiwa kuzindua bendi yake ya muziki wa dansi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Said Fella, alisema bendi hiyo itaongozwa na mwimbaji wake, Dogo Aslay.
“Aslay atakuwa kiongozi wa bendi na hii nafasi ameipata kwa sababu tayari ameishahitimu elimu yake ya kidato cha nne, hivyo hakuna wasiwasi wa kuchanganya muziki na elimu, hivi sasa yuko makini na atajikita zaidi katika muziki,” alisema Fella.
Aidha, aliongeza kuwa bendi hiyo itakuwa ikifanya maonesho yake kila Jumapili, ambako bendi ya Twanga Pepeta itakuwa ikitumbuiza na tayari ameishazungumza na Mkurugenzi wake, Asha Baraka.
Fella aliongeza kuwa Aslay hivi sasa anatamba na kibao kinachokwenda kwa jina la ‘Yamoto’ ambayo inashika kasi katika vituo mbalimbali vya redio nchini.
Wakati huo huo, aliongeza wako katika mazungumzo na uongozi wa Twanga Pepeta ili waweze kufanya onesho maalumu, ambako wasanii watakaokuwepo ni pamoja na kundi zima la TMK, wakiwamo Mh.Temba na Chegge waweze kutoa burudani katika jukwaa moja katika siku watakayopanga.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment